Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatoa ombi la dola bilioni 3.9 kwa ajili ya kusaidia watoto milioni 41 duniani

Mtoto mkimbizi akiwa mbele ya hema lake katika kisiwa cha Lesvos Ugiriki
UNICEF/UN0274758/Haviv VII
Mtoto mkimbizi akiwa mbele ya hema lake katika kisiwa cha Lesvos Ugiriki

UNICEF yatoa ombi la dola bilioni 3.9 kwa ajili ya kusaidia watoto milioni 41 duniani

Msaada wa Kibinadamu

Mamilioni ya watoto wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na mizozo na majanga wanakosa huduma muhimu za ulinzi na hiyvo kuweka usalama na mustakabali wao hatarini, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudmia watoto, UNICEF huku likisema linahitaji ombi la dola bilioni 3.9 ili kusaidia katika shughuli zake kwenye majanga ya kibinadamu.

UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, limesema linatarajia fedha hizo kusaidia watoto milioni 41 kwa mwaka 2019 ambapo fedha hizo zitatumika kusambaza maji safi na salama, lishe, elimu, huduma ya afya na ulinzi katika nchi 59 kote ulimwenguni.

Mathalani, dola milioni 385 kati ya ombi hilo, ni kwa ajili ya programu za ulinzi huku milioni 121 ni kwa huduma za ulinzi kwa watoto walioathirika kutokana na mzozo wa Syria.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “leo mamilioni ya watoto wanaoishi katika mizozo na majanga wanakabiliwa na ukatili wa kusikitisha, dhiki na kiwewe na hatua chanya za kazi yetu ya ulinzi wa watoto haiwezi kusisitizwa zaidi."

Ameongeza kuwa, “Watoto wanapokosa maeneo salama ya kucheza, watoto wanaposhindwa kuungana na familia zao, watoto wanapokosa msaada wa kisaikolojia katu hawataweza kupona makovu ya vita ambayo hayaonekani."

UNICEF inakadiria kuwa takriban watoto milioni 34 wanaoishi kwenye mizozo na majanga wanakosa huduma za ulinzi ikiwemo kuwaepusha na ukatili na kutelekezwa na huduma muhimu,  huku watoto milioni 6.6 wakiwa nchini Yemen, 5.5 nchini Syria na milioni 4 wakiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Kupungua kwa ufadhili na changamoto nyinginezo ikiwemo, upuuzaji wa sheria za kimataifa na uzuiaji wa njia za kufikisha misaada ya kibinadamu, humaanisha kuwa mashirika yanashindwa kulinda watoto  kwa mfano nchini DRC ambako UNICEF ilipokea theluthi moja tu ya dola milioni 21 zilizohitajika kwa mwaka 2018.

UNICEF imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia katika ufadhili huku likionya kuwa ukata huenda ukasababisha baadhi ya watoto kuachwa nyuma katika nyanja mbali mbali.