Lugha 600 za asili duniani hutoweka kila baada ya wiki mbili- UNESCO

Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.
ILO/Marcel Crozet
Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.

Lugha 600 za asili duniani hutoweka kila baada ya wiki mbili- UNESCO

Utamaduni na Elimu

Hii leo huko Paris, Ufaransa, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO linazindua rasmi mwaka huu wa 2019 kuwa mwaka wa kimataifa wa lugha za asili, kufuatia azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2016.

UNESCO inasema lugha ni muhimu siyo tu kwa mawasiliano, elimu na utangamano bali pia inahifadhi tamaduni, maadili na teknolojia za jamii husika.

Hata hivyo licha ya umuhimu huo, Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania Tirso Dos Santos amemweleza Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini humo kuwa kuna tatizo kubwa hivi sasa.

Amesema “watoto wengi zaidi hawazungumzi lugha zao za asili, kwa hiyo uenezaji wa lugha hiyo kutoka kizazi kimoja hadi kingine inapotea, na matokeo yake tunashuhudia lugha 600 za kiasili zinapotea kila wiki.”

Ametolea mfano Tanzania akisema ina lugha za asili 123 kando ya Kiswahili kwa hiyo ni vyema kutunza na kutambua lugha hizo.

Bwana Dos Santos amesema “kwa utambuzi huo unaweza kueneza tabia kadhaa ambazo ni muhimu kwa maendeleo yao. Kuna teknolojia za kiasili ambazo haziwezi kuenezwa kwa lugha ya kiingereza au lugha nyingine za Ulaya. Unahitaji kurejelea lugha hizo ambazo ni ufunguo wa kueneza  ufahamu wa jamii hizo kwa karne na karne.”