Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi nchini Ufilipino

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi nchini Ufilipino

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea leo jumapili kwenye kanisa kuu la Jolo huko Sulu nchini Ufilipino.
 

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mabomu mawili yalilipuka wakati wa ibada kwa nyakati tofauti ndani ya muda mfupi kwenye kanisa hilo katoliki kusini mwa Ufilipino na kusababisha vifo vya watu wapatao 20 na wengine zaidi ya 111 wamejeruhiwa.

Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wake jijini New  York, Marekani leo ameltuma salamu zake za rambirambi kwa wafiwa huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wahusika wa shambulio hilo wafikishwe haraka mbele ya sheria.

Amesisitiza kuwa “Umoja wa Mataifa unaunga mkono serikali na wananchi wa Ufilipino katika harakati zao za kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali.”

Amewasihi waendeleze mchakato wao wa amani kwenye eneo hilo la Bangsamoro.