Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Venezuela barazani, wajumbe wavutana iwapo ni tishio kwa usalama duniani au la!

Wajumbe wa Baraza la Usalama walipokutana Januari 26 2019 kujadili hali ilivyo Venezuela
UN /Manuel Elias
Wajumbe wa Baraza la Usalama walipokutana Januari 26 2019 kujadili hali ilivyo Venezuela

 Venezuela barazani, wajumbe wavutana iwapo ni tishio kwa usalama duniani au la!

Amani na Usalama

Vuta nikuvute kuhusu hali inayoendelea nchini Venezuela kwa sasa, imedhihirika leo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikutana kwenye kikao cha dharura kujadili kinachoendelea wakati huu ambapo  kuna mvutano kati ya Rais Nicolas Maduros wa  nchi hiyo na Juan Guido rais wa Bunge ambaye amejitangaza rais wa muda wa Venezuela.
 

Rais Maduros ambaye aliapishwa tarehe 10 mwezi huu wa Januari kuafuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana anaungwa mkono na baadhi ya nchi ikiwemo Urusi ilhali Marekani na mataifa mengine wanamuunga mkono Bwana Guido wakimtaka aitishe uchaguzi mpya.

Mvutano huo umesababisha  maandamano nchini Venezuela ambapo akihutubia wajumbe wa Baraza hilo, Mkuu wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amesema “hali ya Venezuela inatia wasiwasi mkubwa. Janga hili lililodumu kwa muda mrefu limekuwa na madhara kwa wananchi, kuna mvutano mkubwa kisiasa na kuna hofu kubwa juu ya ongezeko la mahitaji ya kibinamu.”

Amesema janga la Venezuela limeathiri takribani raia milioni 30 ambapo hawana mishahara, kuna uhaba wa chakula, dawa, huduma afya na elimu zimezorota na uzalishaji wa mafuta umeporomoka kwa takribani mapipa laki 5 kwa siku kutoka mwaka 2017 hadi mwaka 2018.

Bi. DiCarlo amesema harakati za kuwezesha mazungumzo kati ya Rais Maduros na upinzani bado hazijazaa matunda “na ghasia zinazondelea zimesababisha vifo vya watu wapatao 20, na wengine wengi wamejeruhiwa.”

Amesema kuna dira tofauti kuhusu mustakabali wa Venezuela hata hivyo, “sote lazima tuongozwe na kile kitakacholeta ustawi kwa wananchi wa Venezuela, na tushirikiane tukidhi mahitaji yao. Tufanye kila tuwezalo kuzuia hali kuwa mbaya zaidi. Lazima tushirikiane tulete suluhu ya kisiasa ambayo itawezesha wananchi kufurahia amani, ustawi na haki za binadamu.”

WAJUMBE WAVUTANA NI WANAOMUUNGA MADUROS NA WALE WA GUIDO

Marekani kwa upande wake iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo ambaye kwa kuzingatia kuwa tayari serikali yake inamuunga mkono Bwana Guido, amekebehi nchi zinazomuunga mkono Rais Maduros akisema zinafanya hivyo ili ziweze kukusanya mabilioni ya dola kutokana na vitegauchumi vyao vya hovyo nchini humo. 

“Leo natoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama waunge mkono mpito wa kidemokrasia na dhima ya Guido katika mchakato huo,” amehitimisha Bwana Pompeo. 

Raia wa Venezuela waliokimbia hali ngumu ya uchumi nchini mwao wakiwa wamewasili kwenye daraja la kimataifa la Rumichaca, ambalo ni eneo la kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Picha ni ya Novemba 2018
UNHCR/Santiago Escobar-Jaramillo
Raia wa Venezuela waliokimbia hali ngumu ya uchumi nchini mwao wakiwa wamewasili kwenye daraja la kimataifa la Rumichaca, ambalo ni eneo la kuingilia Ecuador kupitia Colombia. Picha ni ya Novemba 2018

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vasily Nebenzi amesema wao kwa kuiunga mkono Venezuela na Rais Maduros, “kwanza kabisa tunaonyesha kupinga ukiukwaji mkubwa wa maadili ya sheria za kimataifa, hususan, vifungu vya katiba ya Umoja wa Mataifa, ambayo kwa dhahiri inapinga uingiliaji wa masuala ya ndani ya taifa huru.”

Mjumbe mwingine aliyezungumza ni Afrika Kusini ambayo Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Jerry Matthews Matjila, amesema serikali yao haioni kama kinachoendelea Venezuela ni tisho la amani na usalama duniani akisema Rais Cyril Ramaphosa tayari alishampongeza Rais Maduros kwa kuchaguliwa kwake kuongoza nchi yake.

“Kinachoendelea Venezuela ni masuala ya ndani  ya nchi na Baraza la Usalama halina mamlaka ya kuingilia mambo hayo na kwa kuzingatia uchaguzi ulifanyika kwa usimamizi wa tume inayotambulika,” amesema Balozi Matijla.

 

Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela akihutubia Baraza la Usalama wakati wa kikao kilichojadili hali nchini mwake Pichani ameshikilia katiba ya Umoja wa Mataifa
UN /Manuel Elias
Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela akihutubia Baraza la Usalama wakati wa kikao kilichojadili hali nchini mwake Pichani ameshikilia katiba ya Umoja wa Mataifa

VENEZUELA YAWEKA BAYANA MSIMAMO WAKE

Fursa ikawadia kwa Venezuela kuwasilisha hotuba yake ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje  Jorge Arreaza, alipinga katakata hoja zinazotolewa kuhusu ukosefu wa uhuru na demokrasia kwenye nchi yake. Amelaumu Marekani akisema inataka  kujenga ukuta mpakani na Mexico na kujenga ukuta wa kiitikadi na kimsingi wanarejesha vita baridi.

Akizungumza huku anaonyesha katiba ya Umoja wa  Mataifa, Waziri Arreaza amesema, “kwa jina la Rais Nicolas Maduro, kwa jina la Jamhuri ya Venezuela, kwa jina la wananchi wa Venezuela, na kwa mamlaka ya wengi Venezuela, taasisi na jamii, napenda kusisitiza kuwa Venezula, kama ilivyotajwa kwenye katiba hii, ni huru, na itasalia huru na hakuna mamlaka yoyote bila kujali ukubwa wake inaweza kuamuru mwelekeo au mustakabali wa nchi yetu.”
 

MUUNGANO WA ULAYA NAO WAKANA KUTAMBUA UCHAGUZI WA MEI 2019

Punde baada ya kikao hicho, Sir Alan Duncan wa Uingereza akizungumza na waandishi wa  habari kwa niaba ya Muungano wa Ulaya, EU, amesema hawatambui uchaguzi uliofanyika mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela ambapo Rais Maduros alichaguliwa kwa asilimia 68 kuongoza nchi yake kipindi cha pili cha miaka 6.  Amesema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Badala yake amesema wanaunga mkono Bunge la Venezuela "ambacho ndio chombo cha kidemokrasia na kisheria. Tunaamni kuwa suluhu ya amani na jumuishi ndio muarobaini wa mkwamo wa sasa na zahma ya kijamii ambayo imesababisha.  EU inataka kuitishwa mara moja kwa uchaguzi huru kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya demokrasia na katiba ya Venezuela. Bila kufanya hivyo, EU itachukua hatua zaidi ikiwemo  kutambua uongozi wa nchi kwa mujibu wa kifungu namba 233 cha Katiba ya Venezuela."

Kipengele hicho ni kile kinachompatia madaraka ya kuongoza nchi Rais wa Bunge la nchi hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Baraza la  Usalama kuwa na kikao mahsusi kuhusu Venezuela. Nyakati nyingine Venezuela ilijadiliwa kama ajenda lakini si kama sababu mahsusi ya kikao kama leo.