Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafadhali Msumbiji mwachieni huru mwanahabari Amade Abubacar

Mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa David Kaye
UN /Jean-Marc Ferré
Mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa David Kaye

Tafadhali Msumbiji mwachieni huru mwanahabari Amade Abubacar

Haki za binadamu

Watalaamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hii leo mjini Geneva Uswisi wamezitaka mamlaka nchini Msumbiji kumwachia mara moja mwanahabari Amade Abubacar na pia tuhuma kuwa ametendewa vibaya zichunguzwe.

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa David Kaye na mwenyekiti wa kundi linaloshughulikia masuala dhidi ya watu kufungwa pasipo kufuata utaratibu Seong-Phil Hong wamesema, “Katika wakati ambao vinaongezeka vitisho dhidi ya wanahabari na uhuru wa vyombo vya habari, kukamatwa kwa bwana Abubacar pia tuhuma kuwa ametendewa visivyo hakika inaleta wasiwasi mkubwa. Tunasikitishwa na ukamatwaji na unyanyaswaji ambao kwa bwana Abubacar unahusiana moja kwa moja na kazi yake ya uanahabari na jambo hilo linaweza kuwa na matokeo mabaya katika haki ya uhuru wa kujieleza nchini Msumbiji”

Amande Abubacar ambaye anafanya kazi katika kituo cha redio na Televisheni cha Rádio e Televevisao Comunitária Nacedje na Zitamar News alikamatwa mnamo tarehe 5 Januari mwaka huu wa 2019 katika jimbo la Cabo Delgado alipokuwa akiwahoji watu ambao waliyakimbia mashambulizi yaliyofanywa na vikosi visivyofahamika na vyenye silaha.

Iliripotiwa kuwa alihamishwa hadi katika kambi ya kijeshi ambako aliendelea kushikiliwa bila kuruhusiwa kufanya mawasiliano yoyote kwa siku 12 na kuwa alikuwa akipigwa wakati wa kuhamishwa. Hivi sasa yuko anashikiliwa kabla ya mashitaka katika kituo cha polisi huko wilaya ya Macomia.

Watalaamu wa Umoja wa Mataifa wameendelea kufafanua kuwa wanasheria wa mwanahabari huyo walikataliwa ombi la mteja wao kuachiwa walilolipeleka katika mahakama ya wilaya ya Macomia mnamo tarehe 18 Januari mwaka huu. Kwa taarifa zilizopo hivi sasa ni kuwa bwana Abubacar anatuhumiwa kwa kukiuka sharia ya nchi za kuripoti taarifa nchini Msumbiji.