Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Venezuela hali bado si shwari, UN yataka pande kinzani zizungumze

Watu 233 kutoka Venezuela waondoka Boa Vista katika awamu ya pili ya utaratibu wa kuwahamisha ambapo waomba hifadhi kutoka Venezuela wanawasili katika miji karibu na mipaka wanoahmishwa maeneo mengine ya Brazil. Aprili 5, 2018
© UNHCR/Luiz Fernando Godinho
Watu 233 kutoka Venezuela waondoka Boa Vista katika awamu ya pili ya utaratibu wa kuwahamisha ambapo waomba hifadhi kutoka Venezuela wanawasili katika miji karibu na mipaka wanoahmishwa maeneo mengine ya Brazil. Aprili 5, 2018

Venezuela hali bado si shwari, UN yataka pande kinzani zizungumze

Haki za binadamu

Ghasia zikiendelea nchini Venezuela huku kukiripotiwa vifo vya watu 20 na majeruhi, Kamishna Mkuu wa  haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametaka uchunguzi wa kina wa matukio hayo yatokanayo na vikosi vya usalama kupambana na waandamanaji.

Kwa wiki nzima sasa kumekuwepo na maandamano nchini humo kukiwa na pande mbili ambapo pande moja inamuunga mkono Rais Nicolas Maduro aliyeapishwa wiki iliyopita huku wengine wakikuunga mkono mpinzani wake aliyejitangaza kuwa ni rais wa muda.

Taarifa ya ofisi ya  haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, imemnukuu Bi. Bachelet akisihi pande zote kufanya mazungumzo na kuondoa mvutano unaoendelea.

“Tukio lolote la ghasia linalosababisha vifo au majeruhi lazima lifanyiwe uchunguzi na jopo huru ili kubaini iwapo mamlaka zilitumia nguvu kupita kiasi au iwapo uhalifu umetekelezwa na vikundi vilivyojihami, iwe vinavyounga mkono serikali au vinginevyo,” amesema Bi. Bachelet.

Halikadhalika amesema anatiwa hofu zaidi kuwa hali nchini Venezuela inaweza kuwa mbaya na kushindwa kudhibitiwa na hivyo kusababisha madhara makubwa.

Kwa mujibu wa kamishna huyo mkuu, ofisi yake imepokea ripoti za waandamanaji zaidi ya 350 kutiwa korokoroni, ambapo kati yao hao, 320 walitiwa korokoroni juzi Jumatano.

Kama hiyo  haitoshi, matukio ya uporaji yameshamiri kwenye mji mkuu Caracas ambako kwa wiki hii pekee kumefanyika jumla ya maandamano 180.

“Tafadhali mamlaka za Venezuela hususan vikosi vya usalama vijizuie na viheshimu haki za msingi za kila mtu za kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza. Matumizi holela ya nguvu kupita kiasi ni marufuku kwa mujibu wa sheria,” amesema Bi. Bachelet.

Amesihi pia viongozi wa kisiasa nchini humo waanzishe mazungumzo kwa lengo la kumaliza mvutano na hatimaye kusaka suluhu ya kudumu ya mzozo wa Venezuela ambao umesababisha raia wake kukimbilia ugenini.

Zaidi ya raia milioni 3 wa Venezulea wamekimbia nchi hiyo ilhali mamilioni wengine ni hohehahe kutokana na hali ngumu ya maisha.