Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matukio ya hali mbaya ya hewa yaliathiri zaidi watu milioni 60 duniani kote-Ripoti.

Tarehe 17 Oktoba 2018 nchini Indonesia, Saiful na Gilang wakipita katika kifusi cha msikiti uliodondoka wakiwa wamebeba chuma chakavu wanachotegemea kwenda kukiuza. Nyumba nyingi zilibomoka kutokana na tetemeko la ardhi.
UNICEF/UN0250967/Watson
Tarehe 17 Oktoba 2018 nchini Indonesia, Saiful na Gilang wakipita katika kifusi cha msikiti uliodondoka wakiwa wamebeba chuma chakavu wanachotegemea kwenda kukiuza. Nyumba nyingi zilibomoka kutokana na tetemeko la ardhi.

Matukio ya hali mbaya ya hewa yaliathiri zaidi watu milioni 60 duniani kote-Ripoti.

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu athari za majanga kwa mwaka 2018 inataja matetemeko ya ardhi na tsunami kuchangia asilimia kubwa ya watu 10,373, waliofariki dunia kipindi hicho kutokana na majanga ya asili.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na  kupunguza hatari za majanga, UNISDR imesema kando ya hao waliofariki dunia, watu wengine milioni 61.7 waliathiriwa na majanga ya asili.

Takwimu hizo zinatokana na utafiti wa matukio 281 yaliyorekodiwa na  kituo cha utafiti wa majanga CRED.

Mami Mizutori ambaye ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kupunguza hatari ya majanga amesema, “hakuna eneo la dunia ambalo halikuguswa kutokana na athari za mabadiliko ya kupindukia ya hali ya hewa kwa mwaka jana.  Baada ya matetemeko ya ardhi na tsunami, majanga mengine kama vile mafuriko, ukame, vimbunga na moto wa nyika viliathiri watu milioni 57.3 na nasisitiza zaidi kuwa kama tunataka kupunguza hasara za majanga basi tunatakiwa kuboresha jinsi ya kudhibiti majanga.”

Ikichambua kwa kina matukio hayo, ripoti hiyo imefafanua kuwa majanga kama matetemeko, tsunami na milipuko ya volkano vilivuruga maisha ya watu mulioni 3.4 mwaka jana na kuua watu wengi zaidi kuliko aina nyingine yoyote ya majanga ikiwemo kule Indonesia ambako watu 4,417 walipoteza maisha, Guatemala watu 425 na Papua Guinea 145.

Aidha ripoti imeongeza kuwa mafuriko yaliathiri idadi kubwa ya watu kufikia milioni 35.4 pamoja na watu milioni 23 kule Kerala India. Mafuriko pia yalisababisha vifo 2,859, India ikipoteza watu 504, Japan 220, Nigeria 199 na Korea kaskazini watu 151.

Vimbunga viliathiri watu milioni 12.8 kwa mwaka jana 2018 na kuweka rekodi ya juu ya vifo kufikia 1,593.

Kwa upande wa moto wa nyika barani Ulaya na Amerika kaskazini nao uliweka rekodi ya juu ya vifo 126 nchini Ugiriki, watu 88 Marekani ambako rekodi zinasema ni moto mbaya zaidi kwa zaidi ya karne na ulikuwa wa gharama zaidi kwa kutumia makadirio ya dola bilioni 16.5 za marekani.

Takwimu za CRED zinasema watu milioni 9.3 waliathirika na ukame duniani kote ikiwemo Kenya ambako watu milioni 3 waliathirika na kipindi kirefu cha ukame.