Kunahitajika mabadiliko katika mifumo suala la wakimbizi-Baraza la wakimbizi

Baraza la wakimbizi duniani, WRC limetoa wito kufanyike mabadiliko katika mifumo suala la wakimbizi duniani kwa ajili ya kulinda maslahi ya watu waliolazimika kukimbia ikiwemo walio wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi.
Baraza hilo kupitia ripoti yake iliyozinduliwa Alhamisi wiki hii ikipewa jina, Wito wa kuchukua hatua:Kubadilisha mifumo ya wakimbizi kimatifa, inatoa mapendekezo ya hatua muhimu kwa ajili ya kulinda kundi hilo hususan wanawake na watoto. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuchagiza sauti za wanawake na vijana waliofurushwa, kuunda mfumo wa kufuatilia ambao hawatekelezi wajibu kwenye jamii ya kimataifa, kuimarisha ulinzi wa wakimbizi wa ndani.
Mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo ni rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye punde baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo jijini New York Marekani amezungumza na Idhaa hii na kusema mapendekezo hayo yanahitajika kwa sasa kwani .
(Sauti ya Jakaya Kikwete)
"Dunia mpaka mwaka 2018 imekuwa na watu makundi hayo mawili ambao ni wakimbizi wa ndani na wakimbizi wa nje (walioko nje ya nchi) milioni 68.5 na idadi hii ndio kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote, yaani baada ya vita kuu ya pili hii ndio idadi kubwa ya watu waliohama maeneo yao, wengine wakatoka nje ya nchi lakini wengine wakaishi ndani ya nchi lakini sio kwenye maeneo yale ambayo aylikuwa ni maskani yao."
Akaenda mbali zaidi na kutaja sababu za ongezeko hilo la idadi ya wakimbizi
(Sauti ya Jakaya Kikwete)
"Kuna watu ndani ya nchi zao, viongozi ama wa serikali, (au) wakati mwingine ni wa jamii, kwa sababu watu wanakimbia mateso, wakati mwingine ni uongozi, unakuwa na serikali ambayo ni katili lakini wengine ni sera za kibaguzi ndani ya nchi ambazo zinawabagua watu kama ilivyo Myanmar, wanawakana wale wenzao ambapo wanateswa kwa misingi ya dini, makabila kwa hiyo hayo ndio miongoni mwa mazingira ambayo sio tatizo la kubuni, ni tatizo dhahiri".
Likitilia msisitizo mkataba wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi, baraza hilo limetoa wito kwa hatua katika kukabiliana na janga la uongozi wa kisiasa, pengo la kifedha na uwajibishwaji katika mfumo wa sasa.