Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa ebola watumia uzoefu wao kusaidia wagonjwa DRC

Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.
MONUSCO/Alain Coulibaly
Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.

Manusura wa ebola watumia uzoefu wao kusaidia wagonjwa DRC

Afya

Baadhi ya wagonjwa waliopona ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamechukua jukumu la kujitolea katika vituo vya matibabu ikiwa pia ni mojawapo ya njia ya kulipa fadhila si tu kwa wale waliowahudumia bali pia kwa jamii yao. 

Mjini Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC , anaonekana Faustin Kalivanda, manusura wa ugonjwa wa ebola ambao ulilipuka jimboni humo  mwaka jana.

Yeye ni miongoni mwa manusura 217 wa ebola ambao walipatiwa mafunzo na shirika la afya ulimwenguni WHO ya kushiriki kujitolea katika vituo vya matibabu.

Baada ya kufika kwenye kituo cha afya, hatua ya kwanza ni kunawa mikono, kisha anelekea sehemu ambapo viatu vyake vinasafishwa halafu vipimo vya joto kabla ya kukutana na daktari. 

Manusura huyu anakumbuka watu waliomsaidia kukabiliana na ugonjwa uliosababisha mkewe na mwanae kufariki dunia.

(Sauti ya Faustin Kalivanda)

“Ningependa, kuwashukuru madaktari wote katika kituo cha kutibu ebola na wafanyakazi wote waliohakikisha chumba chote kilikuwa safi, wanasaikolojia waliotupa ushauri kuhusu ugonjwa huo na kutusaidi kurejelea Maisha ya kawaida na wengine wote kwa kutupatia chakula, Kwa hayo yote ningependa kuwashukuru.”

Novemba mosi mwaka uliyopita, Kalivanda aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kugundulika kuwa hana tena virusi vya ebola. 

Ili kuwasaidia manusura wizara ya afya nchini DRC na WHO wanashirikiana kuendesha programu inayolenga mambo matatu: matibabu, biolojia na saikolojia. Dokta Mory Keita ni kutoka WHO

(Sauti ya Dkt. Mory Keita)

“Programu hii inaungwa mkono na WHO katika kuhakikisha ufuatiliaji wa watu waliopona ebola kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kwa sasa WHO imefadhili ukarabati wa vituo vitatu vya ufuatiliako, kimoja Beni, kingine Butembo na kingine Mangina.”

Kila manusura anafuatiliwa kila mwezi kwa kipindi cha miezi sita na kila miezi mitatu kwa mwaka.

Tangu kupona ebola, Kalivanda ameamua kutumia uzoefu wake kuwasaidia wagonjwa wa ebola na anafanya kazi kama mhudumu msaidizi.