Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO na kazi zenye staha kwa wakimbizi wa Syria nchini Jordan

Mjini Amman, Jordan katika kiwanda cha nguo cha Classic Fashion, kikiwa na vyerehani vingi, na wanawake na wanaume wako makini wakishona nguo.
ILO/Video Capture

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Jordan kituo cha kusajili ajira kimekuwa na manufaa makubwa kwa wakimbizi ambao sasa wanajipatia ajira zenye hadhi na utu na hivyo kuweza kukimu siyo tu maisha yao bali pia ya familia zao.

Mjini Amman, Jordan katika kiwanda cha nguo cha Classic Fashion, kikiwa na vyerehani vingi, na wanawake na wanaume wako makini wakishona nguo.

Miongoni mwao ni Fatima Al Atmah, mkimbizi kutoka Syria ambaye aliwasili Jordan na familia yake miaka mitano iliyopita kusaka maisha bora. Miezi minane baadaye kupitia rafiki yake alijulishwa kuhusu kituo cha ajira cha shirika la kazi duniani, ILO ambapo alijisajili na kupata kibali cha kufanya kazi kwenye kiwanda hiki.

(Sauti ya Fatima Al Atmah)

“Nimekutana na watu wapya, ni maisha tofauti. Maisha  yangu yamebadilika kwa sababu nimejifunza kazi mpya na hivi sasa naweza kusaidia familia yangu. Ni jambo jema kimapato na kifikra.”

Fatima na wafanyakazi wengine wakimbizi kutoka Syria na raia Jordan kupitia mpango huu wa ILO wanasaidia kuongeza kiwango cha bidhaa zinazouzwa soko la Ulaya kupitia ushirikiano kati ya Jordan na Muungano wa Ulaya, EU, makubaliano ambayo yamelegeza masharti ya kanuni za biashara kule bidhaa zinapotengenezwa.

Maha Kattaa ni afisa wa ILO nchini Jordan anasema bado kuna changamoto za kupata soko la bidhaa hizo Ulaya hivyo wanasaidia kufanikisha hilo na changamoto nyingine ni …

(Sauti ya Maha Kattaa)

“Kupata wafanyakazi kutoka Syria kufanya kazi kwenye hivi viwanda. Kupitia vituo vyetu vya ajira wasaka ajira kutoka Syria na Jordan wanaweza kuunganishwa na hizi kampuni.”