Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlioko Davos, haki za binadamu kwenye biashara zisienguliwe- Wataalamu

Taswira ya nje kwenye eneo ambalo kunafanyika jukwaa la kiuchumi duniani  huko Davos, Uswisi
WEF/Valeriano Di Domenico
Taswira ya nje kwenye eneo ambalo kunafanyika jukwaa la kiuchumi duniani huko Davos, Uswisi

Mlioko Davos, haki za binadamu kwenye biashara zisienguliwe- Wataalamu

Haki za binadamu

Jukwaa la uchumi duniani likianza vikao vyake leo huko Davos, nchini Uswisi, jopo la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesihi viongozi wanaoshiriki mkutano huo kuhakikisha kuwa haki za binadamu ni msingi mkuu wa utandawazi.

Jopo hilo limesema wito huo unazingatia ukweli kuwa  utandawazi umeengua watu wengi hususan maskini na hivyo, “majadiliano yoyote yale ya kusongesha uchumi ni lazima yapatia kipaumbele haki za watu maskini.”

Mkutano huo wa mwaka wa jukwaa hilo la uchumi limejikita katika maudhui ya jinsi ya kushughulikia changamoto za zama za sasa za maendeleo ya kidijitali.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na mwenyekiti wao Surya Deva, wajumbe hao wametoa wito kwa kampuni za biashara kuheshimu haki za binadamu katika operesheni zao zote kwa kuwa “suala hilo la kupatia kipaumbele haki za binadamu linaonekana kutokuwepo kwenye ajenda za Davos za kuangazia utandawazi.”

Wajumbe hao wamesisitiza kuwa ipwao haki za binadamu hazitajumuishwa ipasavyo kwenye mjadala wao, hitimisho la jukwaa litakuwa ni marejeo ya kuwa na utandawazi ambao umekuwa ni tatizo kwa wengi duniani.

Bwana Deva ametumia taarifa hiyo kuwakumbusha wajumbe juu ya uwepo wa kanuni za mwongozo wa biashara na haki za binadamu ambazo zitasaidia utandawazi uwe na manufaa kwa wote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatarajiwa kuhutumia mkutano huo wa Davos  Alhamisi hii ya tarehe 24 mwezi huu wa Januari.