Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakabali bora wa ajira uzingatie maslahi ya binadamu na si vinginevyo- Ripoti

Miaka 100 ya shirika la kazi duniani, ILO.
ILO/Marcel Crozet
Miaka 100 ya shirika la kazi duniani, ILO.

Mustakabali bora wa ajira uzingatie maslahi ya binadamu na si vinginevyo- Ripoti

Masuala ya UM

Kamisheni ya kimataifa kuhusu mustakabali wa ajira duniani leo imesihi serikali kuweka mikakati kwa lengo la kushughulikia changamoto zinazotokana na mabadiliko makubwa katika sekta ya ajira ili hatimaye ajira siyo tu iwe ni ya utu bali pia iwe endelevu.

Kamisheni hiyo iliyoundwa na shirika la kazi duniani, ILO ikiwa na wajumbe 27 imetoa wito huo kupitia ripoti yake iliyozinduliwa leo huko Geneva, Uswisi baada ya uchunguzi wa miezi 15 ikichambua changamoto za ajira ziletwazo na teknolojia mpya, mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya mwenendo wa makundi ya watu duniani.

Ikiwa na wenyeviti wenza Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na Waziri Mkuu wa Sweden Stefan Löfven, kamisheni hiyo baada ya uchunguzi imependekeza dira ambamo kwayo binadamu ni kitovu cha uwekezaji wa uwezeshaji binadamu, kazi za taasisi, ajira endelevu na yenye utu.

akizungumza huko Geneva, Uswisi hii leo Rais Ramaphosa amesema “ukosefu wa usawa unaongezeka, ukosefu wa ajira na umaskini vimenasa mamia ya mamilioni ya watu duniani kote. Kwa ufupi mustakabali wa jamii zetu  unategemeea jinsi ambavyo tunashughulikia fursa na changamoto zinazohusiana na mazingira ya kazi. tunahitaji kutunga upya sera sambamba na hatua ambazo zitakuwa na matokeo yanayopatia kipaumbele binadamu.

Ni kwa mantiki hiyo ripoti hiyo imekuja na mapendekezo 10.

Mapendekezo 10 ya ajira yenye utu na hadhi

Mathalani ajira ambayo inalinda haki za msingi za mfanyakazi kwa upande wa ujira unaomwezesha kuishi, saa za kazi zenye ukomo na mazingira safi na salama kwenye kazi.

Halikadhalika hakikisho la hifadhi ya jamii tangu mtu anapozaliwa hadi uzeeni, mafao ambayo yanamwezesha kukimu mahitaji yake, fursa ya kujiendeleza na kuboresha stadi zake.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder (kulia) akiwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo huko Geneva, Uswisi hii leo 22 Januari 2019.
ILO/Marcel Crozet
Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder (kulia) akiwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo huko Geneva, Uswisi hii leo 22 Januari 2019.

Kamisheni pia inataka usimamizi bora wa mabadiliko ya teknolojia ili yawezesha kuchagiza ajira yenye utu na yasiyoengua wengine.

Suala pia la muundo mpya wa mfumo wa biashara ili kuchagiza uwekezaji wa muda mrefu na pia uwekezaji mkubwa kwenye uchumi usioharibu mazingira na vijijini.

Mwenyekiti Mwenza Ramaphosa na umuhimu wa uamuzi wa haraka na dhati

Rais Ramaphosa amesema amesema “fursa lukuki zinasubiri iwapo watu wataboresha mazingira ya kazi na kuziba pengo la jinsia kwenye ajira. Lakini hii  haiwezi kujileta bila kuamua. Bila uamuzi wa dhati tutakuwa tunaota ndota kwenye dunia ambayo pengo la ukosefu wa usawa na ukosefu wa uhakika wa maisha linazidi kuwa kubwa.”

Uzinduzi wa ripoti hiyo ni sehemu ya mwanzo wa maadhimisho ya shirika la kazi duniani, ILO kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake ambapo shirika linatathmini kile kilichofanyika na mwelekeo wa baadaye.