Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa nishati ya mafuta mjini Gaza ni hatari kwa sekta ya Afya-WHO

Uhaba wa nishati Gaza umeleta changamoto kubwa na uhaba wa umeme. Picha hii ni ya mwaka 2014 huko Abeer al Nemnen kutoka kambi ya wakimbizi ya Ash Shati kwenye ukanda wa Gaza.
OCHA
Uhaba wa nishati Gaza umeleta changamoto kubwa na uhaba wa umeme. Picha hii ni ya mwaka 2014 huko Abeer al Nemnen kutoka kambi ya wakimbizi ya Ash Shati kwenye ukanda wa Gaza.

Uhaba wa nishati ya mafuta mjini Gaza ni hatari kwa sekta ya Afya-WHO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO hii leo kupitia wavuti wake limeonesha wasiwasi wake kuwa uhaba wa nishati unaoendelea huko ukanda wa Gaza usipotafutiwa suluhisho unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa maisha na afya za wagonjwa ambao matibabu yao yanahitaji uwepo wa nishati hiyo muda wote.

Taarifa hiyo imesema hospitali 14 za umma zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa umeme na kupungua kwa haraka kwa akiba ya mafuta yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuendeshea jenereta wakati wa kukatika kwa umeme wa gridi ya taifa kulikochukua muda mrefu.

Hospitali kadhaa ambazo zimeathirika na hali hiuyo tayari zimeanza kujiendesha kwa kutumia mbinu ya mgao wa umeme na pia kupunguza baadhi ya huduma wakati wa mgao zikiwemo za usafi, upigaji picha za matibabu, kufua na hata uandaaji wa vyakula. Upasuaji unaohitaji umeme umepunguzwa na wauguzi na madaktari wanaonya kuwa kuna uwezekano wa kuzifunga baadhi ya wodi.

WHO imeeleza pia kuwa mamia ya wagonjwa wakiwemo vichanga na watoto ambao maisha yao yanategemea mathalani uwepo wa huduma za kuondoa maji kwenye figo, vifaa vya kuwapatia joto watoto waliozaliwa kabla ya wakati na vifaa vya hewa katika vyumba vya uangalizi maalumu na vingine vya kuokoa maisha, vitaathirika moja kwa moja.

Dkt Gerald Rockenschaub, ambaye ni mkuu wa ofisi ya WHO katika Ukingo wa Magharibi na Gaza anasema, “uhaba mkubwa wa mafuta unaathiri sana uwezo mfumo wa afya huko Gaza, ambao unakabiliwa na uhaba wa muda mrefu wa dawa, vifaa vya matibabu na umeme. Bila suluhisho la haraka ili kushughulikia vifaa vya dharura katika hospitali, wagonjwa wengi katika mazingira hatarishi watawekwa katika hatari zaidi.  Kufuatia ziara zetu kwenye vituo kadhaa vya walioathirika huko Gaza, tunatoa wito kwa pande zote kuhakikisha kuwa huduma za kuokoa maisha zimehifadhiwa "

Hivi sasa akiba ya mafuta inategemewa kuweza kumudu kutoa huduma za muhimu tu za kitabibu kwa siku chache zijazo kulingana na saa ambazo umeme utazimwa.

WHO imetoa wito kwa mamlaka za Gaza na pande zote -pamoja na wadau kuwajibika na kuhakikisha haki ya afya na haki za kila mtu kufikia huduma za kiafya.