Si kweli wakimbizi na wahamiaji Ulaya husababisha magonjwa ya kuambukiza- Ripoti

Wahamiaji na wakimbizi wanaokwenda barani Ulaya wako hatarini zaidi kupata magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza kuliko wenyeji wa nchi ambako wanafikia.
Hiyo ni kwa mujibu wa wa ripoti ya kwanza kabisa iliyotolewa leo na shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Ulaya ikilenga kubaini pengo la huduma za afya na nini kifanyike kuhakikisha wakimbizi na wahamiaji wanaishi maisha yenye afya bora.
Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya, Dkt. Zsuzsanna Jakab amesema hali ya hatari ya kupata magonjwa inakumba wakimbizi na wahamiaji wakati huu ambapo mifumo ya sasa ya kisiasa na kijamii inahaha kukabiliana na madhila ya wakimbizi kwa njia chanya zaidi.
Akitaja walichobaini, Dkt. Jakab amesema, “kuna hatari ndogo sana kwa wakimbizi na wahamiaji kuambukiza wenyeji magonjwa ya kuambukiza, hii ni moja ya fikra potofu ambayo nimetaka kuwaeleza. Wakati magonjwa ya kuambukiza yanahusishwa moja kwa moja na ukimbizi na uhamiaji, kuna ongezeko la uelewa kuwa baadhi ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanahitaji kushughulikiwa.”
Miongoni mwa magonjwa ambayo si ya kuambukiza lakini yananyemelea zaidi wahamiaji na wakimbizi, ni kisukari ambapo kundi lililo hatarini zidi ni wanawake. "Ripoti inasema kuwa magonjwa hayo kama kisukari yanatokana na ukweli kuwa lishe inakuwa ya mashaka na fursa ya mazoezi inakuwa ni finyu."
Ripoti hiyo pia imebaini ukweli halisi kuhusu idadi ya wahamiaji kwenye ukanda wa Ulaya ambapo tofauti na fikra potofu ya kwamba idadi ya wahamiaji wa kimataifa na wakimbizi kuwa ni asilimia 10 ya wakazi wote wa ukanda wa huo ambayo ni wahamiaji wa kimataifa milioni 90.7. Kati yao hao, wakimbizi ni chini ya asilimia 7.4 na hivyo kuondoa fikra potofu ya kwamba idadi ya wahamiaji ni mara 3 au 4 zaidi ya ukweli halisi.
Amezungumzia pia hatari ya watoto wakimbizi kupata magonjwa kwa kuwa wanapofurushwa makwao hawafuati tena mfumo wa chanjo. "Kwa hiyo ni muhimu sana kwa nchi wanachama ambazo zinawapokea ziwapatie haraka huduma ya chanjo kwa mujibu wa ratiba ya nchi hiyo inayowapokea.”
Ripoti hiyo inatokana na utafiti wa nyaraka 13,000 na kile ambacho kimefikiwa na nchi za Ulaya katika kuendeleza afya ya wakimbizi na wahamiaji na iliandaliwa kwa ushirikiano na taasisi ya taifa ya afya, uhamiaji na umaskini nchini Italia, INMP.