Uhasama wa kibiashara huenda ukaathiri uchumi wa nchi zinazoendelea-Ripoti

21 Januari 2019

Ripoti ya mwaka 2018 ya hali ya uchumi na makadirio duniani inaonesha kuwa kuna ukuaji mkubwa kiuchumi, lakini kuna hatari na uwezekano wa kiwango hicho kutofikiwa kufikiwa kutokana na  uhasama wa biashara ambao umeimarika na kuathiri biashara kimataifa na ajira.

Hayo yamesemwa na Elliott Harris, msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na mchumi mkuu kwenye idara ya uchumi na masuala ya kijamii, ya Umoja huo, DESA, wakati wa mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Bwana Harris amesema uhasama wa kibiashara umekuwa na athari mbaya na kwamba..

“Tunatarajia kuwa ukuaji wa biashara utakuwa mdogo mwaka 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018. Iwapo uhasama huo utaendelea, ukizingatia kuwa ushiriki katika biashara kimataifa ni njia moja ya nchi zinazoendelea kushiriki katika ukuaji kimatifa. Iwapo kuna jambo litakwamisha biashara hiyo basi itakuwa na athari mbaya kwa uwezo wa nchi hizo kuimarisha ukuaji na maendeleo endelevu.”

Kuhusu Afrika, Msaidizi huyo wa katibu mkuu  amesema uchumi wa Afrika umekuwa chanya katika miaka ya hivi karibuni na umekuwa kwa kasi kubwa lakini  ukuaji wa pato la taifa hauendani sawa na kasi au ongezeko la idadi ya watu na hivyo kutia hofu iwapo bara hilo litaweza kutokomeza umaskini ifikapo mwaka 2030.

Kwa hivyo tuna changamoto mbili, mosi ni kuhakikisha kuwa tunasalia au hata kuimarisha uchumi wa Afrika kwa ujumla, uchumi wa kila nchi kwa sababu sio nchi zote zinafanya vizuri kiuchumi, pili changamoto kubwa Afrika kama ilivyo katika mataifa mengine ni ukosefu wa usawa. Iwapo tutaweza kusuluhisha hilo tutaweza kuimarisha ukuaji na kupunugza umaskini kwa ujumla yanayoshuhudiwa miongoni mwa makundi yaliyotengwa”.

Bwana Harris amesisitiza kuwa nyingi ya changamoto ambazo zinashuhudiwa katika dunia leo hii zinahitaji ushirikiano wa mataifa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na hivyo kusisitiza kuwa ni muhimu kurekebisha kasoro za  ushirkiano wa kimataifa badala ya kukumbatia utaifa.

Ukuaji wa uchumi kimataifa

Ukuaji wa kiuchumi kimataifa unatarajiwa kusalia kwenye asilimia 3.0 mwaka 2019 na 2020, hatahivyo, mwenendo wa ukuaji wa kiuchumi unaongeza kwa upande mwingine hatari ambazo huenda zikaathiri maendeleo katika maeneo mengi ya dunia. 

Kwa mujibu wa ripoti, uchumi wa kimataifa unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo huenda zikaathiri shughuli za kiuchumi na kusababisha athari kubwa na za muda mrefu kwa ukuaji. Changamoto hizo ni kuimarika kwa uhasama wa kibiashara na hali ya kifedha kimatiafa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

 Utekelezaji wa Agenda 2030

Ukuaji wa kiuchumi unaficha hatari za muda mfupi ambazo huenda zikaarthiri ukuaji uchumi na kudumaza maendeleo ya muda mrefu ambapo ripoti inasema hali hiyo huenda ikahatarisha ufikiaji wa mengi ya malengo ya maendeleo endelevu kwa nchi zilizo na hatari zaidi ikiwemo zenye pengo kubwa ya usawa wa kiuchumi na viwango vya juu vya deni. 

Halikadhalika kufuatia mabadiliko kwenye sera kote ulimwenguni, misukosuko kutoka nje inaweza kuwa na athari kubwa na za muda mrefu katika ukuaji wa uchumi na hali ya jamii kiuchumi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter