Ghasia Zimbabwe, watu waripotiwa kuuawa, UN yataka mbinu mbadala kusaka suluhu

18 Januari 2019

Nchini Zimbabwe, kitendo cha vikosi vya usalama kutumia nguvu kupita kiasi ikiwemo risasi za moto kudhibiti waandamanaji wanaopinga hali nguvu ya uchumi na kijamii, ikiwemo kuongezeka kwa bei ya mafuta, kimesababisha ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa itoe tamko la kuelezea wasiwasi wake juu ya mwelekeo wa hatua hiyo.

Msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi amesema badala ya kutumia nguvu, serikali isake mbinu za kushauriana na wananchi juu ya malalamiko yao na iache mara moja kukamata waandamanaji.

Maandamano hayo yalianza Jumatatu ambapo watu wanapinga hatua zilizochukuliwa na serikali za kubana matumizi sambamba na kuongeza bei ya mafuta hali ambayo imekuwa na madhara kwa biashara, huduma pamoja na kaya ambazo tayari zina hali ngumu.

Habari zinasema kuwa waandamanaji hao wamekuwa wakichoma matairi ya magari na kuweka vizuizi barabarani ili kuzuia mabasi yasisafirishe watu wanaokwenda kazini. “Baadhi ya majengo yamechomwa moto huku kukiwepo na ripoti za uporaji ambapo polisi walilazimika kutumia nguvu na risasi za moto,” amesema Bi. Shamdasani.

Ameongeza kuwa kuna taarifa za uhakika  za vifo akiwemo afisa wa polisi na watu wengi wamejeruhiwa na wengine kuwekwa korokoroni huku ikiripotiwa kuwa polisi wanafanya msako wa nyumba kwa nyumba.

Bi. Shamdasani amesema watu zaidi ya 600 wanashikiliwa na polisi wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati mashuhuri huku huduma ya mtandao wa intaneti ikikumbwa na kasoro.

“Tunaunga mkono wito wa tume ya haki za binadamu nchini Zimbabwe wa kutaka serikali ianzishe mazungumzo ya kitaifa yakijumuisha watu kutoka pande mbalimbali ili kusaka suluhu ya kudumu ya changamoto za kiuchumi zinazokabili nchi hivi sasa,” amesema Bi. Shamdasani akisema pia uchunguzi wa ghasia ufanyike na wanaoshikiliwa kiholela kwa kuandamana kwa amani waachiliwe huru.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud