Kampuni ya mitindo mjini Jakarta inawapa nafasi wakimbizi kujifunza biashara na kufikia ndoto zao

18 Januari 2019

Mradi wa Benang wa mavazi ya mitindo nchini Indonesia unawapatia fursa adimu wakimbizi ambao si tu fursa kupata ajira ni adimu bali pia katika maeneo mengine hawaruhusiwi kufanya kazi. 

Mradi huu wa Benang unaendeshwa na mjasiriamali mzaliwa wa Indonesia Franka Soeria ambaye pia ni mwanzilishi mwenza wa wiki ya maonesho ya mavazi marefu kwa wanawake, maonesho ambayo yanafanyika katika miji mbalimbali ulimwenguni

Soeria alianzisha mradi huu wa Benang baada ya kukutana na shirika la kuhudumia wakimbizi la UNHCR na akasikia changamoto zilizokuwa zinawakumba wakimbizi walioko mijini.

(Sauti ya Franka Soeria)

“Benang ni uzi wa kushonea kwa hivyo tunaweza kuziunganisha pande hizi mbili kwa pamoja yaani jamii na wakimbizi. Kwa hivyo watakuwa kitu kimoja. Kwa kuwa pamoja wanaweza kutengeneza kitu kikubwa”

Ahmad Musawer Faiz mwenye umri wa  miaka 21 alikimbia nchi yake ya Afghanstan mwaka 2015 wakati Taliban walipoishambulia nyumba yake. Alifika Indonesia akiwa peke yake na mara zote amekuwa anavutiwa sana na mitindo.

(Sauti ya Ahmad Musawer Faizi)

“Sasa ninafikiri ninaweza kukuza maarifa yangu na kuyafanya kuwa makubwa. Mradi huu kwangu ni kama ufunguo wa ndoto zangu. Walinipa ufunguo ili niweze kufungua mlango na ndoto zangu zitimie”

Mradi huu ulianza mwezi Septemba mwaka jana wa 2018 na unawafundisha wakimbizi watano wasichana na mmoja wa kiume kuhusu tasnia ya mitindo na baadhi ya kazi zao tayari zimeoneshwa katika maonesho makubwa mjini Paris, Ufaransa.

Soeria ana matumaini ya kuupanua mradi huu na anawahamsasisha watu wengine wenye miradi ya tofauti kuwapa wakimbizi fursa kama hizi za mafunzo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter