Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 890 waliuawa DRC wakati wa ghasia mwezi uliopita

Mapigano ya kikabila huko DRC yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao.
UNHCR/Colin Delfosse
Mapigano ya kikabila huko DRC yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao.

Watu 890 waliuawa DRC wakati wa ghasia mwezi uliopita

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema watu wapatao 890 waliuawa katika ghasia zilizogubika maeneo ya magharibi mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC katikati mwa mwezi uliopita wa Disemba.

Taarifa ya ofisi hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imenukuu vyanzo vya uhakika vya habari vikisema kuwa mauaji  hayo ni kati ya tarehe 16 na 18 mwezi uliopita na ni katika vijiji vilivyoko eneo la Yumbi jimbo la Mai-Ndombe.

Chanzo ni kile kinachoelezwa kuwa ni mapigaon kati ya makabila ya Banunu na Batende ambapo ripoti zinadokeza kuwa watu wengine 82 walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.

Halikadhalika nyumba 465 na majengo yalichoma moto, zikiwemo shule mbili za msingi, kituo cha afya, soko na tume huru ya uchaguzi nchini humo.

Mamia ya watu walisaka hifadhi kwa kuvuka mto Congo ambapo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC imesema imeanzisha  uchunguzi wa taarifa hizo wakati huu ambapo mahakama nazo zinachunguza.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa  Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema ni muhimu sana taarifa hizi za kutisha za ukatili zikachunguzwa haraka na haki ipatikane kwa manusura.

Kamishna huyo amesema ofisi yake iko tayari kutoa msaada kwenye uchunguzi na kuhakikisha vitendo kama hivyo havitokei tena.