Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Palestina yakabidhiwa uenyekiti wa kundi la G77 na China.

Hafla ya makabidhiano ya uenyekiti wa G-77 kutoka kwa Misri kwenda kwa taifa la Palestina.
UN Photo/Manuel Elías
Hafla ya makabidhiano ya uenyekiti wa G-77 kutoka kwa Misri kwenda kwa taifa la Palestina.

Palestina yakabidhiwa uenyekiti wa kundi la G77 na China.

Masuala ya UM

Leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa  mjini New York Marekani, Palestina imekabidhiwa uenyekiti wa kundi la nchi 77 yaani G-77 na China. 

Akizungumza katika mkutano ambao umehudhuriwa pia na Rais wa Palestina Mahamoud Abbas, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na kuipongeza Palestina ametoa wito kwa nchi zote kuongeza nguvu kupambana na changamoto zinazoukumba ulimwengu, “ Ninatarajia kuendelea kufanya kazi pamoja na G77 na China katika mwaka huu wa 2019 chini ya uongozi wa kihistoria wa taifa la Palestina. Palestina na wananchi wake wana uzoefu wa moja kwa moja wa changamoto na masuala yanayoikabili dunia. Mwaka 2019 utakuwa mwaka muhimu kwa ajili ya juhudi zetu za pamoja kutokomeza umaskini, kupunguza kutokuwepo kwa usawa na kujongea katika kushirikishana na uchumi endelevu”

Aidha Bwana Guterres amesema mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanatakiwa kuongozwa na nchi za kundi la G77 zikiwa katika mstari wa mbele.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesema nchi yake imepata heshima ya kuchukua uenyekiti wa kundi la 77 na China akisema,“Ninayo heshima kwa niaba ya watu wa palestina na taifa la Palestina kuchukua uenyekiti wa G77 na China kwa mwaka 2019. Hapana shaka ni wajibu mkubwa ambao Palestina itautekeleza kwa utu, kuwajibika na kujitolea kwa kulinda maslahi ya kundi na kuimarisha nafasi za wanachama katika Umoja wa Mataifa”

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa amesema, “Huu ni wakati wa kihistoria na njia tuliyopita kufika hapa haikuwa rahisi. Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa umefanya kazi ngumu, kuanzia katika uamuzi wa kuitoa Palestina katika kuwa mwanachama mwangalizi asiyepiga kura uamuzi uliofanyika mwaka 2012 hadi  uamuzi wa mwaka jana Oktoba wa kuifanya Palestina  kutekeleza urais”

Aidha Bi Espinosa ameongeza kwamba leo tunaweza kusherehekea uhamisho huu wa Urais wa Kundi la 77 na china bila shaka ni ushindi wa ushirikiano wa kimataifa na Ushahidi wa umuhimu wa jukumu la kidemokrasia zaidi na uwakilishi wa Umoja wa Mataifa.

Palestina ilichaguliwa na kundi hilo kushika wadhifa huo mwaka jana ambapo nalo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura mwezi Oktoba kulipatia taifa hilo hadhi  ya uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa kwa wakati huu ambapo linashikilia wadhifa huo ili iweze kutekeleza majukumu yake. Kwa kawaida Palestina ina hadhi ya uangalizi katika Umoja wa Mataifa.

Uenyekiti wa kundi hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wanachama ndani ya Umoja wa Mataifa, unazunguka baina ya mataifa wanachama kutoka Afrika, Asia-Pasifiki, Amerika ya Kusini na Karibea na hudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kupitia kundi hilo, nchi hizo za kusini zinachagiza maslahi yao ya kiuchumi na uwezo wa mashauriano kwenye masuala nyeti ya kimataifa ndani ya Umoja wa Mataifa na huchagiza pia ushirikiano baina yao.

Kundi la nchi 77 lilianzishwa tarehe 15 mwezi Juni mwaka 1964 na mataifa 77 kutoka nchi zinazoendelea ambazo zilitia saini azimio la pamoja la nchi 77 zinazoendelea.

Utiaji saini wa azimio hilo ulifanyika mwishoni mwa mkutano wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na maendeleo mjini Geneva, Uswisi.

Ijapokuwa wanachama wa kundi hilo sasa wameongezeka na kufikia 134, bado kundi hilo limesalia na jina lake la G77 ili kuzingatia historia yake.