Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa ombi la dola milioni 296 kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi

Wakimbizi kutoka Burundi wakipika chakula kutumia kuni
UNICEF/Seck
Wakimbizi kutoka Burundi wakipika chakula kutumia kuni

UNHCR yatoa ombi la dola milioni 296 kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake, leo wametoa ombi la dola milioni 296 kwa ajili ya kutoa msaada wa dharura mwaka huu wa 2019 kwa wakimbizi 345, 000 wa Burundi walioko nchi jirani.

Kwa mujibu wa tarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa UNHCR,wakimbizi wa Burundi ni moja ya kundi lililosahaulika zaidi duniani na mwaka 2018 lilipata ufadhili mdogo zaidi. Kwa mantiki hiyo uhaba huo unashuhudiwa katika nchi jirani zinazowahifadhi wakimbizi ikiwemo, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,DRC,  Rwanda na Uganda ambako kunashuhudiwa upungufu wa mgao wa chakula, ukosefu wa dawa, msongamano katika shule na makazi hayatoshelezi mahitaji.

UNHCR imesema ufadhili zaidi unahitajika ili kuweza kukidhi mahitaji ya msingi ya wakimbizi, huku watoto ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya wakimbizi ni waathirika wakubwa na wengi waliwasili katika nchi wanakohifadhiwa baada ya kutenganishwa na wazazi.

Halikadhalika UNHCR imesema watoto hao wanakabailiwa na changamoto mablimbali ikiwemo, kuwatafutia walezi, msongo wa mawazo, upatikanaji wa elimu hususan baada ya shule ya msingi ni ndoto kwa wengi. Aidha wanawake na wasichana wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia na kingono kufuatia makazi duni au ukosefu wa vifaa vya kupika ambavyo huwalazimu kutoka kambini na kutembea nje ya kambi na hivyo kuhatarisha usalama wao.

Wakati hali ya usalama imeimarika kwa kiasi fulani Burundi, wakimbizi 57,000 wamerejea nyumbani tangu katikati mwa mwaka 2017 hatahivyo, UNHCR inaamini kwamba hali bado haijatengamaa wakati huu ambapo wastani ya wakimbizi 300 wanakimbia kutoka Burundi kila mwezi.

Kwa mantiki hiyo wametoa wito kwa nchi jirani kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka Burundi.

Mwaka 2018 ni asilimia 35 tu ya ombi la dola milioni 391 lilifadhiliwa na hviyo UNHCR imetolea wito jamii ya kimatifa kuimarisha juhudi zake na ufadhili ili waweze kuwasilisha misaada ya dharura kwa wakimbizi kutoka Burundi.

 

TAGS: UNHCR, Burundi, wakimbizi