Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio Kenya, UN yaonyesha mshikamano

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres
UNFCCC Secretariat/James Dowson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres

Shambulio Kenya, UN yaonyesha mshikamano

Amani na Usalama

Kufuatia taarifa za mashambulizi kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi hii leo Jumanne, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea mshikamano na wananchi wa Kenya pamoja na serikali yao.

Bwana Guterres ametoa tamko hilo la mshikamano kabla ya kuhutubia mkutano wa kukabidhi Palestina uenyejikiti wa kundi la nchi 77 na China, G-77.

“Niruhusu kwanza nipaze sauti  yangu na kuelezea mshikamano na wananchi wa Kenya, serikali yao na Rais wa Kenya na kulaani vikali shambulio la kikatili ambalo ndio kwanza tumepata taarifa zake."

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernande Espinosa katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa G-77  amesema,

“Niruhusu kwanza nitume rambirambi zangu za dhati kwa serikali na watu wa Kenya kwa shambulio la leo la kigaidi. ninashikamana na waathirika wa tukio hilo la ghasia na familia zao. Nalaani vikali vitendo hivi vya ghasia za kupita kiasi ambazo hazina maelezo yoyote.".

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ambaye naye alikuwepo kwenye mkutano huo wa makabidhiano ya uenyekiti wa kundi la nchi 77 na China kwa Palestina alitumia sehemu ya hotuba yake kuonyesha mshikamano na Kenya akisema kuwa,

"tunaelezea mshikamano wetu, kwa niaba yako, na Rais wa Kenya na wananchi wa Kenya. Tunalaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea leo mjini Nairobi ambalo limesababisha vifo na majeruhi. Kwa pamoja tunalaani ugaidi na aina zake zote, bila kujali unapotokea au wanaotekeleza. Ugaidi ni ugaidi. Sote lazima tulaani ugaidi na aina zake zote."

Kwa upande msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani amesema wanaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo na watatoa taarifa zaidi kadri zinavyopatikana.

Tweet URL

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa magari mawili yaliyokuwa na vilipuzi yaliingia katika eneo la hoteli ya DusitD2 huko River drive takribani kilometa 3 kutoka katikati mwa mji mkuu Nairobi na hatimaye kukasikika milipuko na milio ya risasi.

Taarifa zaidi kuhusu tukio hilo tutachapisha kadri zinavyopatikana.