Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea Palestina kuongoza G-77, Mahmoud akutana na Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) akikutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kulia) akikutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani

Kuelekea Palestina kuongoza G-77, Mahmoud akutana na Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amekuwa na mazungumzo na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kabla kufanyika kwa mkutano wa kundi la nchi 77, G-77 na China hapo kesho ambapo Palestina inachukua uenyekiti wa kundi hilo.

Bwana Guterres ametumia fursa hiyo ya mazungumzo kupongeza Palestina kwa kuchukua uenyekiti wa G-77 akitakia mafanikio mema kundi hilo.

Halikadhalika amesisitiza kuwa suluhu ya mataifa mawili ndio muarobaini sahihi wa amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati.

Mara baada ya Palestina kuchaguliwa kuongoza kundi hilo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba mwaka jana lilipitisha azimio namba A/73/L.5 la kupatia taifa hilo haki za nyongeza na upendeleo wa ziada  kutokana na kushika wadhifa huo.

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 146, huku Marekani, Australia na Israeli zikipiga kura za hapana ilhali mataifa 15 hayakupiga kura kuonyesha msimamo wowote.

Kwa mujibu wa azimio hilo, Palestina ambayo kwa kawaida ni mwanachama mwangalizi asiyepiga kura, sasa wakati wa mwaka huu wa 2019  ikiwa mwenyejiti wa kundi la nchi 77 itakuwa na haki ya kutoa tamko, kuwasilisha mapendekezo na kujitambulisha kwa niaba ya G-77 na kuwasilisha hoja.

Uenyekiti wa kundi hilo lenye idadi kubwa zaidi ya wanachama ndani ya Umoja wa Mataifa, unazunguka baina ya mataifa wanachama kutoka Afrika, Asia-Pasifiki, Amerika ya Kusini na Karibea na hudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kupitia kundi hilo, nchi hizo za kusini zinachagiza maslahi yao ya kiuchumi na uwezo wa mashauriano kwenye masuala nyeti ya kimataifa ndani ya Umoja wa Mataifa na huchagiza pia ushirikiano baina yao.

Kundi la nchi 77 lilianzishwa tarehe 15 mwezi Juni mwaka 1964 na mataifa 77 kutoka nchi zinazoendelea ambazo zilitia saini azimio la pamoja la nchi 77 zinazoendelea.

Utiaji saini wa azimio hilo ulifanyika mwishoni mwa mkutano wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na maendeleo mjini Geneva, Uswisi.

Ijapokuwa wanachama wa kundi hilo sasa wameongezeka na kufikia 134, bado kundi hilo limesalia na jina lake la G77 ili kuzingatia historia yake.