Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usalama unatishia hatua zilizopigwa Afrika Magharibi na Sahel-Chambas

Mohamed Ibn Chambas
Picha ya UN /Eskinder Debebe
Mohamed Ibn Chambas

Ukosefu wa usalama unatishia hatua zilizopigwa Afrika Magharibi na Sahel-Chambas

Amani na Usalama

Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi, Mohammed Ibn Chambas leo ameliambia Baraza la Usalama  la umoja huo jijini New York, Marekani kuwa hatua zimepigwa katika kuwekeza demokrasia kwenye eneo hilo na ukanda wa Sahel licha ya changamoto za kiusalama.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu kazi za Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika magharibi na ukanda wa Sahel (UNOWAS), Chambas amesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita kumekuwa na matokeo chanya katika kufanyika chaguzi mbalimbali ikiwemo, uchaguzi mkuu uliofanyika Mali, uchaguzi wa maeneo Mauritania na wa bunge Togo na uchaguzi mashinani ulioratibiwa na Cote d Ivoire.

Hata hivyo, Bwana Chambas amesema "licha ya hatua mujarabu katika kuchagiza amani katika ukanda huo, kuna umuhimu wa juhudi endelevu kushughulikia mambo muhimu tatanishi yanayoibuka kuhusu uchaguzi ili kuzuia na kukabiliana na mgogoro kutokana na uchaguzi na kusaidia mashauriano jumuishi kama kiungo muhimu kwa ajili ya jamii jumuishi."

Chambas ametaja baadhi ya changamoto kubwa  ikiwemo, katika ziwa Chad ambako kumekuwepo na mashambulizi zaidi yanayotekelezwa na Boko Haram katika miezi ya hivi karibuni na migogoro kati ya wakulima na wafugaji vinaendelea kwa kiwango kidogo. 

Nako nchini Burkina Faso kufuatia ongezeko la visa vya usalama hali ya hatari ilitangazwa katika maeneo 13 kaskazini, magharibi na mashariki akiongeza kuwa "nchini Niger licha ya kuratibiwa kwa vikosi cya ulinzi na usalama bado wanakabiliwa na changamoto maeneo ya magharibi na kusini."

Mkuu huyo wa UNOWAS amesema mzunguko mwingine wa uchaguzi katika ukanda huo utakuwa ni mtihani kwa ajili ya kuchagiza demokrasia na kuhakikisha mazingira yanayowezesha haki zote za bindamu kuheshimiwa na itakuwa muhimu kwa chaguzi hizo zifanikiwe kwa ajili ya kulinda utulivu katika ukanda huo.

Bwana Chambas amesema UNOWAS inahitaji msaada ili kufanikisha utulivu katika ukanda wa Afrika Magharibi na Sahel.