Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manusura wa ebola DRC wasaidia kulea watoto yatima

Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.
MONUSCO/Alain Coulibaly
Kituo cha matibabu ya Ebola katika Hospitali mjini Beni, jimboni Kivu ya kaskazini, DRC.

Manusura wa ebola DRC wasaidia kulea watoto yatima

Afya

Nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mlipuko wa mwaka wa jana wa ebola kwenye majimbo ya Equateur na Kivu Kaskazini yameacha takribani watoto 400 yatima au kutengwa na familia yao na hivi sasa manusura wa ugonjwa huo amechukua hatua ya kuwalea. 

Katika kituo kimoja cha kutibu Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC anaonekana Kavira, mwanamke manusura wa ugonjwa wa Ebola akiwa anabembeleza mtoto Josue baada ya kumnywesha maziwa. Kavira  aligua Ebola lakini alipona na anasema…

“Nilipona kwasababu nilitunzwa vizuri. Baada ya kupona waliniuliza, kama wanavyouliza manusura wote wa ebola, kama umepona basi nije hapa kulea watoto ambao mama zao ni wagonjwa.”

Kituo hiki kina kilichofunguliwa mwezi Novemba mwaka jana kina majengo yenye michoro ya kuvutia kwa watoto na  hadi sasa kimeshalea zaidi ya watoto wachanga 20.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF na wadau wake wanashirikiana na manusura wa Ebola kulea watoto ambao wazazi wao bado wanapatiwa matibabu dhidi ya ebola.

“Nauelewa huu ugonjwa na nafahamu kile ambacho mama yake anapitia. Iwapo sitamtunza vyema huyu mtoto, mtoto hatokuwa na furaha. Napaswa kumlea vyema kama ambavyo mama  yake angalifanya. Na mimi nafurahi sana nikicheza naye, tunalala, namlisha chakula, nafurahi sana.”

Jambo la kusikitisha ni kwamba mama mzazi wa Josue alifariki dunia kwa ebola na baba yake angali anapata matibabu.