Heko Said Abdullahi Deni kwa kuchaguliwa Rais wa Puntland

9 Januari 2019

Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Raisedon Zenenga amepongeza kuchaguliwa kwa Said Abdullahi Deni kuwa Rais mpya wa eneo la Puntland kaskazini-mashariki mwa Somalia.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM imemnukuu pia Bwana Zenenga akimpongeza makamu wa Rais Ahmed Elmi Karash ambao kwa pamoja walichaguliwa siku ya Jumanne.

Maeneo matano ya Somalia, ambayo ni Puntland, Galmudug, Hirshabelle, Jimbo la Kusini-Magharibi na Jubaland yako kwenye mchakato wa uchaguzi ambao ulioanza mwezi Novemba mwaka jana na utaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Bwana Zenenga pia amepongeza tume ya uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi huru, wa haki na kwa njia ya amani akisema kuwa “tunatarajia kufanya kazi kwa karibu na utawala wa Rais Deni huko Puntuland. Tunampongeza pia Rais aliyemaliza muda wake Abdiweli Mohamed Ali ‘Gaas’ pamoja na uongozi wake kwa kuweka mazingira yaliyowezesha tume ya uchaguzi kuwa na mchakato wa amani  wa uchaguzi.”

Kwa sasa Bwana Zenenga ndiye anakaimu ukuu wa UNSOM kufuatia uamuzi wa wiki iliyopita wa serikali ya shirikisho nchini Somalia wa kumtaka aliyekuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo na mkuu wa UNSOM, Nicholas Haysom aondoke nchini humo.

Bwana Haysom alikuwa anatuhumiwa na serikali kwa kuingilia masuala ya ndani ya  nchi ikiwemo kuhoji kukamatwa kwa aliyekuwa naibu mkuu wa Alshabaab mapema mwezi uliopita, sambamba na ugombea wake kwenye uchaguzi wa urais jimbo la Kusini-Magharibi kuondolewa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres sambamba na Baraza la Usalama walitoa taarifa kuhusiana na tukio hilo la Bwana Haysom kutakiwa kuondoka nchini humo.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter