Mafuriko katika makazi ya wakimbizi Lebanon ni tabu juu ya tabu

9 Januari 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR linatoa msaada wa dharura kwa wakimbizi wa Syria walioko nchini Lebanon baada ya mvua kubwa kunyesha katika nchi hiyo.

Katika bonde la Bekaa nchi Lebanon  kwenye makazi ya wakimbizi kutoka Syria, wanaonekana watoto wakijaribu kuvuka katika mitaa ya mahema yaliyozungukwa na maji kila upande nje na ndani. Watoto wakitembea wanajishikiza katika mahema yaliyochanika na wengine wameamua kutembea tu katika maji kwani hakuna paliposalia, na juhudi  za kujaribu kukwepa maji zimeshagonga mwamba.

Hiba Fares, afisa habari wa UNHCR anasema shirika limekuwa likijaribu kuzisaidia familia zilizoathiriwa na mafuriko. Ameongeza kuwa mahema ya baadhi ya watu yamechanika au kukatika na wengine wamelazimika kuhamia katika mahema ya majirani au ndugu zao.

“Tumekuwa tukipitapita na kujaribu kusaidia pale tunapoweza. Maji mengi yaliingia kwenye mahema. Hakuna mashaka kuwa hali ni mbaya”

UNHCR inakadiria kuwa wakimbizi 50,000 wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi yapatayo 850 wanaweza kuathirika na mafuriko. Hakuna majeruhi ambao wameripotiwa hadi kufikia sasa.

Wakimbizi wanaonekana katika video wakiwa wamebeba magodoro na mahema, Hiba Fares, afisa habari wa UNHCR  anaeleza,

“Leo tunajaribu kila tuwezalo kuwapatia msaada na mahitaji ya muhimu kama magofdoro na blanketi ili waweze angalau kupata joto wakati wa usiku”

Nchini Lebanon, maisha ni mahangaiko ya kila siku kwa zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Syria ambao wana vyanzo kidogo au hawana kabisa vyanzo vya mapato. Hakuna kambi rasmi za wakimbizi na matokeo yake wakimbizi hao wametapakaa katika maeneo mbalimbali mara nyingi wakitumia malazi na familia nyingine za wakimbizi katika maeneo yaliyojaa watu wengi sana.

Tangu mwaka 2011, Zaidi ya watu milioni 5.6 wameikimbia Syria na kuingia katika nchi jirani au mbali Zaidi. Wengine wameishia katika katika mipaka ya nchi yao. Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wameomba dola bilioni 5.5 za kimarekani ili kuweza kutoa misaada ya kibinadamu duniani kote mewaka huu.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter