Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pedersen aanza jukumu lake kuhusu Syria

Balozi Geir Pedersen mjumbe mpya maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria,katika picha hii iliyopigwa mwaka 2014.
UN /Loey Felipe
Balozi Geir Pedersen mjumbe mpya maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria,katika picha hii iliyopigwa mwaka 2014.

Pedersen aanza jukumu lake kuhusu Syria

Amani na Usalama

Mwanadiplomasia nguli kutoka Norway Geir Pedersen ameanza rasmi jukumu lake la kuwa mjumba maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, ofisi yake ikiwa mjini Geneva, Uswisi.

Bwana Pedersen anachukua nafasi ya Staffan de Mistura, aliyehudumu wadhifa huo kwa zaidi ya miaka minne na kung’atuka mwezi Desemba mwaka jana.

Anakuwa ni mtu wa nne kushika wadhifa huo baada ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa hayati Kofi Annan aliyeshika wadhifa huo na kuachia ngazi mwaka 2012 na kisha Lakhdar Brahimi kuanzia mwaka 2012  hadi 2014.

Mzozo wa Syria ulianza kama maandamano ya amani mwezi Machi mwaka 2011 dhidi ya Rais Bashar al-Assad na hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 400,000, huku takribani milioni 11.7 wakikimbia makwao, wakiwemo zaidi ya milioni 5.5 waliosaka hifadhi nchi jirani.

Bwana Pedersen ambaye amezaliwa Oslo Norway mwaka 1955 ameshika nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia ikiwemo mwakilishi wa kudumu wa Norway kwenye Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.

Halikadhalika amewahi kuwa mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon kati ya mwaka 2007 hadi 2008 na pia mwakilishi binafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la kusini mwa Lebanon tangu mwaka 2005 hadi 2007.