Onyesha mshikamano na wakimbizi kwa kutembea kilometa bilioni 2

8 Januari 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetangaza leo kuanza kwa kampeni ya kimataifa ya watu kutembea na kufikisha umbali wa kilometa bilioni 2 ambazo wakimbizi hulazimika kutembea kila mwaka. Taarifa zaidi na Arnold Kayanda.

Kampeni hiyo iliyopatiwa jina, kilometa bilioni 2 kufikia usalama, itachagiza watu kuchukua hatua binafsi kushikamana na wakimbizi.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa vitendo hivyo kwa pamoja vitaashiria ujasiri na uthubutu wa wakimbizi na kampeni inalenga kuchangisha dola milioni 15 kwa ajili ya kuwezesha uandikishaji wa wakimbizi na huduma za mapokezi ikiwemo chakula, maji, makazi na huduma msingi za afya.

Hatua hii ya UNHCR inatokana na shirika hilo kufuatilia safari za wakimbizi katika maeneo tofauti kote ulimwenguni na kujumuisha na ndipo lilipata kwamba wakimbizi hutembea kilometa bilioni 2 mpaka kufikia kituo cha kwanza cha maeneo salama.

Mathalani mwaka 2016, wakimbizi kutoka Syria walitembea kilometa 240 ili kufika Uturuki. Wakimbizi kutoka Sudan Kusini walifunga safari ya kilometa 640 kufika Kenya na wakimbizi wa kabila la rohingya kutoka Myanmar walitembea kilometa 80 hadi Bangladesh.

“Kila siku vitendo vya watu ambao wamejitolea kuimarisha maisha ya wakimbizi vinatupa moyo, ikiwemo jamii zinazowahifadhi, wafadhili, biashara na wafanyakazi wa kujitolea. Kampeni hii itawezesha watu kushiriki kupitia vitendo ambavyo wanavifanya kila siku iwe ni kutembea, kuendesha baiskeli au kukimbia,” amesema naibu kamishna mkuu wa UNHCR, Kelly T. Clements.

Ameongeza kuwa, “wakati huu ambapo kuna mitazamo tofauti kuhusu wakimbizi ni muhimu kujikumbusha safari hatari ambazo wakimbizi huchukua, safari ambazo wanalazimika kufunga”.

Mwaka 2019 watu kutoka nchi 27 za bara la Afrika, Asia Amerika ya kati na Kaskazini, Ulaya na Mashariki ya kati watashiriki kampeni hiyo ikiwemo watu binafsi, watu maarufu, wakimbizi na wafanyakazi wa UNHCR. 

Akizungumzia kampeni hiyo balozi mwema wa UNHCR na muigizaji, Ben Stiller amesema wakimbizi hukimbia ukatili na mateso na wanajizatiti kuishi na hivyo ameelezea mshikamano wake na wakimbizi nakutoa wito watu wamuunge mkono. 

Kwa taarifa kuhusu kampeni na kushiriki, tembelea  wavuti,  www.stepwithrefugees.org 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter