Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 430 zahitajika kusaidia wananchi CAR 2019

Mjini Bambari nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, operesheni za kibinadamu zinatatizwa na barabara mbaya, uhalifu, uporaji na machafuko ya makundi ya wanamgambo wenye silaha
OCHA/Gemma Cortes

Msaada wa Kibinadamu

Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR inaendelea kukabiliwa na janga la kibinadamu ambapo mtu mmoja kati ya wanne ni mkimbizi wa ndani au mkimbizi, imesema  Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA.

OCHA katika taarifa iliyotolewa leo huko Bangui, mji mkuu wa CAR, imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada na ulinzi mwaka huu imeongezeka kutoka watu milioni 2.5 hadi 2.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Kati ya hao, watu milioni 1.9 wanahitaji msaada wa dharura na haraka.

Kwa mantiki hiyo OCHA kwa pamoja na serikali ya CAR, imezindua leo ombi kwa ajili ya mpango wa msaada kwa mwaka 2019, la dola milioni 430.7 kusaidia watu milioni 1.7 walio hatarini zaidi nchini CAR.

Kwa kuzingatia malengo matatu, mpango huo unatarajiwa kuokoa maisha, kuimarisha ulinzi wa watu walioathirika na kuhakikisha utu na wakati huo huo wakiwezesha uwasilishaji wa huduma muhimu za kuokoa maisha.

Ombi hilo limetolewa wakati huu ambapo hali ya kiusalama inadorora huku kukishuhudiwa ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa misaada ambapo visa elfu moja vya kiulinzi viliripotiwa kwa mwaka 2018 na idadi ya visa dhidi ya watoa huduma ya misaada imeongezeka kutoka watu 337 mkwa 2017 hadi 396 mwaka 2018.

Licha ya hali ngumu katika sekta zote, mratibu wa misaada ya kibinadamu, CAR, Bi. Najat Rochdi amesisitiza hali ya kujitolea na ujasiri wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu katika kuleta matumaini kwa watoto, wanawake na wanaume waathirika wa mzozo.

“Mwaka 2019, hatutaendeleza juhudi ila tutaziimarisha ili kuepukana na hali mbaya zaidi. Kwa mantiki hiyo natoa wito kwa wasamaria wema wasisahau Jamhuri ya Afrika ya Kati na watuunge mkono kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza hatua za miaka iliyopita na kutoa msaada wa kibinadamu,” amesema Bi Rochdi.

Mwaka 2018, OCHA ilipokea ufadhili wa dola 253.9 na kuwezesha uwasilishaji wa misaada kwa watu 900,000 katika mpango wa kuwasilisha misaada ya kibindamu.