Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau yahaha kusaidia raia wa DRC waliokimbilia Congo-Brazaville

Wakimbizi kutoka DRCongo wakiondoka Congo Brazaville
MONUSCO/Sylvain Liechti
Wakimbizi kutoka DRCongo wakiondoka Congo Brazaville

UNHCR na wadau yahaha kusaidia raia wa DRC waliokimbilia Congo-Brazaville

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasaidia mamlaka nchini Jamhuri ya Congo ili ziweze kupatia msaada wa kibinadamu wakimbizi wapatao 16,000 ambao wamewasili nchini humo kufuatia mapigano ya kikabila huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva Uswisi, Andrej Mahecic amesema mapigano hayo ya kikabila yametokea mwishoni mwa mwezi Desemba huko Yumbi, jimbo la Mai-Ndombe mashariki mwa DRC.

“Uhasimu wa muda mrefu kati ya kabila la Banunu na wale wa Batende ulisababisha mapigano mapya yaliyosababisha makumi kadhaa ya watu kuuawa ilhali majeruhi 150 waliwasili Congo-Brazaville na majeraha yao,” amesema Mahecic.

Bwana Mahecic amesema wakimbizi wengi wao wanawake na watoto wa  kabila la Banunu bado wanaendelea kuwasili wilaya za Makotipoko na Bouemba nchini Congo-Brazaville ambako mamlaka za nchi hiyo kwa kushirikiana na UNHCR zinawapatia huduma za matibabu, chakula na vifaa vingine muhimu.

Kwa mujibu wa wakimbizi hao, makazi yao huko DRC  yamechomwa moto na watu wameuawa ilhali wengine wanahofu kuwa mapigano haya

yatazidi kuendelea.

UNHCR inasema hili ni wimbi kubwa zaidi la wakimbizi kutoka DRC kuingia Congo-Brazaville tangu mwaka 2009 ambapo takribani raia 130,000 wa DRC waliingia Congo-Brazaville wakisaka hifadhi kufuatia mapigano ya kikabila kwenye jimbo la zamani la Equator.

Tathmini ya hivi karibuni iliyofanywa huko Yumbi ambako kumeripotiwa mapigano ya kikabili,  ilibaini kuwa zaidi ya nyumba 450 zimechomwa moto ilhali watu wana uhitaji mkubwa wa misaada muhimu kama vile chakula, huduma za afya na makazi.

Mamlaka za Congo-Brazaville zimeomba rasmi msaada ili kusaidia wakimbizi hao ambapo UNHCR na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP na wadau wengine wanaratibu harakati za kutoa misaada hiyo.

Ingawa juhudi hizo zinaendelea, UNHCR inasema bado wakimbizi wanaishi kwenye mazingira magumu wakipata hifadhi kwa wenyewe ambao tayari nao wanakabiliwa na uhaba wa maji, chakula na huduma za afya.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu nayo yanakabiliwa na changamoto kwa kuwa baadhi ya maeneo yanafikika kwa njia ya mto, mvua za na mafuriko navyo vikiwaweka hatarini wakazi hao kukumbwa na magonjwa kama vile malaria na mengineyo.

Jamhuri ya Congo, au Congo-Brazaville inahifadhi wakimbizi 60,000 wengi wao kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, DRC na Rwanda.