Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Uganda kwa maandalizi fanisi dhidi ya Ebola- WHO

Muuguzi akiandaa kitanda kwa ajili ya mtu anayehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Bwera, Wilaya ya Kasese karibu na mpaka wa DR Congo.3 September 2018.
UNICEF/UMichele Sibiloni
Muuguzi akiandaa kitanda kwa ajili ya mtu anayehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola katika Hospitali ya Bwera, Wilaya ya Kasese karibu na mpaka wa DR Congo.3 September 2018.

Heko Uganda kwa maandalizi fanisi dhidi ya Ebola- WHO

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amepongeza  hatua zilizochukuliwa na serikali ya Uganda za maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola iwapo utalipuka kwenye maeneo hatarishi zaidi nchini humo.

Dkt.  Tedros amesema hayo leo  kwenye mkutano uliofanyika katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda mjini Kampala ukihudhuriwa na viongozi waandamizi wa seriakli akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Sam Kutesa.

Taarifa ya WHO imemnukuu Dkt. Tedros akisema kuwa mikakati ya Uganda ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa inatambuliwa kwa ufanisi wake akipongeza hatua ya serikali ya taifa hilo la Afrika Mashariki ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola akisema itaokoa maisha ya wahudumu wa afya hususan wale walio mstari wa mbele zaidi katika utoaji tiba.

Amegusia pia shukrani zilizotolewa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kutokana na msaada wa Uganda wa kuimarisha vituo vya udhibiti wa maambukizi kwenye maeneo ya mipakani.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma ya afya kwa wote nchini Uganda ili kuzuia magonjwa miongoni mwa wananchi akisema kuwa uimarishaji wa afya na kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza ni msingi wa kufikia azma ya huduma ya afya kwa wote.

Naye Waziri Mkuu wa Uganda, Dkt. Ruhakana Rugunda ameshukuru jitihada za WHO za kusaidia Uganda akisema kuwa chochote kile ambacho nchi hiyo imeweza kufanikiwa katika masuala ya afya ya umma ni kutokana na mchango wa WHO akitolea mfano harakati za kudhibiti Ebola.

Kufuatia mlipuko wa Ebola huko maeneo ya mashariki mwa DRC, Uganda imechukua hatua kadhaa kuhakikisha inajikinga na gonjwa hilo ikiwemo kutoa chanjo kwa wahudumu wa afya, kuwachunguza wasafiri kwenye maeneo ya mpakani na kuchunguza damu kutoka kwa watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.