Kilio cha WFP kwa operesheni zake Sudan Kusini chaitikiwa na China

3 Januari 2019

Huko nchini Sudan Kusini, mchango wa dola milioni 7 kutoka China kwa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP utasaidia shirika hilo kununua vyakula kama vile mchele, maharagwe na vinginevyo kwa ajili ya mgao wa mlo kwa wanafunzi shuleni sambamba na kwa zaidi ya watu 126,000 kwenye maeneo yaliyokumbwa na mzozo na ukosefu wa chakula. 

WFP kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini imesema kuwa mchango huo umekuja wakati muafaka wakati ambapo shirika hilo linahitaji fedha ili kuendelea na operesheni zake za mgao wa chakula kwa watu milioni 5.2 ambao wanatarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula kati ya mwezi huu wa Januari hadi mwezi machi mwaka huu.

Mkurugenzi wa WFP nchini humo Adnan Khan ametolea mfano mgao wa chakula shuleni akisema ni uwekezaji wa kipekee kwa ajili ya kizazi kijacho na kwa taifa hilo kwa ujumla.

Halikadhalika amesema mchango huo utaokoa shirika hilo wakati huu ambapo wakimbizi wa ndani nao wanaanza kurejea nyumbani kufuatia makubaliano mapya ya amani.

Hata hivyo amesema ili kuweza kuendelea na operesheni zao za mgao wa chakula kwa miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu, WFP itahitaji dola milioni 179.

WFP imemnukua Balozi wa China nchini Sudan Kuini He Xiangdong akisema kuwa mchango wao ni sehemu tu ya ahadi ya serikali yake ya kusaidia serikali ya Sudan Kusini na mashirika ya kibinadamu ili yawezeshe taifa hilo kukabiliana na njaa.

Mwaka jana pekee, WFP ilifikia watu milioni 5 katika maeneo yenye janga kwa kuwapatia tani 259,000 za chakula na dola milioni 24.5 za kuwawezesha kununua mahitaji muhimu.

Kwa mujibu wa WFP mchango wa China katika operesheni za shirika hilo umeongezeka kwa kiasi kikubwa hivi karibuni ambapo michango yam waka 2015 na 2017 iliwezesha kununua takribani tani 4,600 za chakula zilizokuwa mgao kwa watu 290,000.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter