Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi Mogadishu katu hayanizuii kuendesha biashara ya hoteli- Mfanyabiashara

Ndani ya hoteli ya Makkah Al Mukarama kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu
UNSOM video screen capture
Ndani ya hoteli ya Makkah Al Mukarama kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Mashambulizi Mogadishu katu hayanizuii kuendesha biashara ya hoteli- Mfanyabiashara

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Somalia licha ya mashambulizi yanayoripotiwa mara kwa mara dhidi ya miundombinu ya kijamii zikiwemo hoteli, wananchi wameitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka mashambulio ya aina hiyo yasiwazuie azma yao ya kujenga taifa lao kwa maendeleo yao na taifa lao. 

Kutana na Abdikadir Abdi Hassan, al maaruf kama Gurey Hajji. Raia huyu wa Somalia ni mkazi wa mji mkuu Mogadishu, akiwa amejikita katika sekta ya hoteli.

Kupitia video mahsusi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, zinazoonyesha harakati za wananchi kusongesha taifa lao, Hajji anasema kuwa aliingia katika sekta ya huduma za hoteli mwaka 1985 kwa kujenga hoteli iitwayo Makkah Al-Mukarama.

Hata hivyo serikali ya Somalia ilipoporomoka mwaka 1991..

“Tulikimbia nchi na tuliporejea Somalia niliamua kurejea katika kazi yangu ya awali. Nilikarabati hoteli hii ya Makkah Al-Mukarama mwaka 2012. Hata hivyo ilishambuliwa tena mara nne. Hata hivyo, katu sikukata tamaa. Kwa kuwa nilikuwa najihusisha na sekta ya hoteli hata kabla ya serikali kuporomoka, nillidhani kuwa hoteli ni moja ya vitu ambavyo vinarejesha uzuri wa eneo na imani ya watu.”

Mmiliki huyo wa hoteli ya Makkah Al-Mukarama yenye ghorofa tatu anajinasibu kuwa uendeshaji wa hoteli ni jambo ambalo ana ujuzi nalo mkubwa sana na kutokana na uwezo wake wa uendeshaji ameweza hata kutoa fursa za ajira kwa watu..

“Watu 100 wanafanya kazi kwenye hoteli hii. Familia 100 zinalishwa kutokana na hoteli hii. Aidha ni pahala ambapo watu wanaweza kukutana na kuwa pamoja. Kila siku watu 100 wanaondoka majumbani mwao wanakuja hapa kufanya kazi, marafiki wengi pia wanakutana hapa. Pana shughuli nyingi ,huwezi kujisikia kutovutiwa. Ndio maana napenda kazi hii.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.