Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan fanyeni uchaguzi ulio huru na wa haki:UNAMA

Mamia wakiwa katika mchakato wa upigaji kura za kuwachagua wabunge huko Kandahar, Afghanistan tarehe 27 Oktoba 2018. Uchaguzi wa Urais umetangazwa kufanyika julai 2019.
UNAMA / Mujeeb Rahman
Mamia wakiwa katika mchakato wa upigaji kura za kuwachagua wabunge huko Kandahar, Afghanistan tarehe 27 Oktoba 2018. Uchaguzi wa Urais umetangazwa kufanyika julai 2019.

Afghanistan fanyeni uchaguzi ulio huru na wa haki:UNAMA

Amani na Usalama

Ujumbe wa msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA umepongeza hatua ya tume ya uchaguzi nchini humo IEC kutangaza ratiba ya uchaguzi wa rais ambao umepangwa kufanyika mwezi julai mwaka wa 2019.

Aidha katika taarifa ambayo imetolewa leo mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, UNAMA imekaribisha ufafanuzi wa kalenda ya uchaguzi.

Taarifa ya UNAMA inaongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unaelewa fika tangazo la tarehe mpya  limefuatia mashauriano ya kina na wadau wote ambao wameonyesha hamu ya kuwa na uchaguzi unaoaminika na ulio wazi.

Pia Umoja wa Mataifa, unakubaliana na tathimini ya tume huru ya uchaguzi kuwa, muda zaidi unahitajika ili kujifunza  kutoka katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwaka 2018 na hivyo kufanya matayarisho yanayofaa.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa unaisihi tume ya uchaguzi nchini humo, kuchapisha kalenda ya uchaguzi yenye ufafanuzi zaidi na kutoa maelezo ya kila mara kuhusu mchakato huo. Kwa kuwa maelezo zaidi yaliyoko katika kalenda ya uchaguzi yanatoa taarifa zaidi kwa wananchi kuhusu uchaguzi huo.

Umoja wa Mataifa unaamini kuwa uchaguzi wa rais ni muhimu mno kwa mustakbali mzuri wa Afghanistan na kuuboronga hakutakubalika.

Pia Umoja wa Mataifa unaishauri tume inayohusika na malalamiko ya uchaguzi kutekeleza wajibu wake kwa kufanya uchunguzi unaofaa  kuhusu malalamiko yanayojitokeza kutokana na uchaguzi wa wabunge. Na wale wote walio na malalamiko kuhusu mizengwe  katika uchaguzi wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwa tume inayohusika na malalalmiko ya uchaguzi, kwa kuzingatia katiba ya nchi pamoja na sheria za uchaguzi wa Afghanistan.Umoja wa Mataifa unamkumbusha kila mtu kuwa hakuna mwenye haki ya kuvuruga  mchakato wa uchaguzi pamoja na ushwari wa nchi kupitia uchochezi pamoja na kutoa vitisho.

Umoja wa Mataifa unaahidi kuendelea kuratibu na kushirikiana na jamii ya kimataifa kuhusu msaada  unaohitajika kwa taasisi za uchaguzi nchini humo ili kuwepo uchaguzi unaoaminika, na ulio wazi na pia ukiwa unakubalika.

Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa wadau wote wanawajibika kwa kufanyika uchaguzi wenye haki na kuwa na mchakato wa uchaguzi ulio salama.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.