Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chakula cha msaada Yemen chauzwa sokoni- WFP

Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.
WFP/Marco Frattini
Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Chakula cha msaada Yemen chauzwa sokoni- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakuka WFP linataka kukomeshwa mara moja kwa hatua ya kupelekwa kwingine msaada wa chakula nchini Yemen baada ya kugundua mchezo mchafu unaofanywa katika mji mkuu wa Sana’a  na sehemu zingine zinazosimamiwa na kundi la Houthi wa kupeleka chakula maeneo yasiyokuwa yamelengwa na msaada huo.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Roma Italia, WFP inasema kuwa uchunguzi wao kwa walengwa wa msaada waliosajiliwa unaonyesha kama watu wengi ambao walikuwa wanapashwa kupokea mgao wao katika mji wa Sana’a hawajapata mgao huo.

Taarifa inaongeza kuwa katika maeneo mengine watu wenye njaa wamekuwa wakinyimwa mgao wao kamili wa chakula.

Watu mamilioni kadhaa nchini Yemen wanategemea chakula cha msaada kuweza kuishi kutokana na mapigano ya wao kwa wao kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa Houthi.

Matumizi mabaya ya chakula cha msaada yamejulikana katika uchunguzi uliofanywa na WFP katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, uchunguzi ambao ulichochewa na taarifa kuwa chakula cha msaada kinauzwa wazi sokoni katika mji wa Sana’a.

Uchunguzi ulifichua kuwa mchezo huo unafanywa  na shirika la ndani ambalo lilipewa jukumu la kushughulikia na kusambaza chakula cha msaada. Shirika hilo ni sehemu ya wizara ya Elimu katika mji wa Sana’a ambao unadhibitiwa na wahouthi.

Katikati ya mwaka huu wa 2018, Meli kubwa ya mizgo ilishusha shehena ya ngano katika bandari ya Al-Saleef kaskazini magharibi mwa Yemen. Mzigo huo ungetosha kuwa chakula kwa watu milioni 1 kwa miezi miwili
WFP
Katikati ya mwaka huu wa 2018, Meli kubwa ya mizgo ilishusha shehena ya ngano katika bandari ya Al-Saleef kaskazini magharibi mwa Yemen. Mzigo huo ungetosha kuwa chakula kwa watu milioni 1 kwa miezi miwili

 

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, David Beasley anasema kuwa, “ tabia hii ni sawa na wizi wa kuondoa chakula mdomoni kwa watu wenye njaa. Kwa wakati huohuo, watoto wanafariki dunia  nchini Yemen kwa kuwa hawana chakula cha kutosha.Haya ni makosa na ni lazima yakomeshwe mara moja.”

WFP inasema ina ushahidi wa picha zikionyesha kama malori yakipakia, kiharamu,  na kuondoka katika maghala ya chakula hicho. Pia wamegundua kuwa majina ya wanaopaswa kupewa chakula yanabadilishwa na maafisa wa mahali hapo na pia kughushi nyaraka. Iligundulika kuwa baadhi ya watu ambao hawapaswi kupata chakula hicho hupewa, huku kingine kikiuzwa wazi katika soko za mji huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, amewataka viongozi wa wahouthi mjini Sana’a wachukue hatua za haraka kukomesha mchezo huo na kuona kama chakula kinawafikia wale tu ambao wanastahili kukipata la sivyo, “tutasitisha kufanya kazi na waliofanya njama za kuwanyima walio wengi chakula  wanachohitaji mno.”

Kwa sasa WFP inaongeza juhudi zake za msaaada wa chakula ili kuweza  kufikia walio na njaa wapatao milioni 12 nchini Yemen. Bila chakula watu milioni 20 wanaweza kukumbwa na mgogoro wa njaa katika nchi ambayo imevurugwa na vita vya wenye we kwa wenyewe tangu mwaka 2015.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.