Kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani-Guterres

28 Disemba 2018

Wakati wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakihesabu saa kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na majimbo unaotarajiwa kufanyika jumapili hii desemba 30, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yake aliyoitoa kupitia msemaji wake hii leo mjini New York Marekani, amewasihi mamlaka nchini DR Congo, viongozi wa kisiasa wa pande zote, tume ya uchaguzi CENI na jumuiya za kijamii kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira yasiyo na vurugu kusudi siku ya uchaguzi wapiga kura wote wanaostahili waweze kupiga kura zao kwa amani.

Aidha Katibu Mkuu Guterres amewahimiza wananchi wa DRC kuitumia fursa hii ya kihistoria kushiriki katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia za nchi yao.

Guterres amewakumbusha wadau wote wa uchaguzi huo kuwa wana jukumu muhimu la kufanya katika kuzuia vurugu za uchaguzi kwa kuepuka aina yoyote ya kuchochea na hali ya kukwamisha kwa maeno au matendo yao. Pia ametoa wito kwa kila mmoja kulinda na kuhakikisha ufikaji salama katika vituo vya afya katika maeneo yaliyoathirika na ebola.

Vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia ahadi ya Umoja wa Mataifa kusaidia makabidhiano ya madaraka kwa amani katika Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter