Wataalamu wa UN waitaka Sudan kuacha kutumia nguvu kubwa kuzuia maandamano ya amani.

Hii leo mjini Geneva, Uswisi, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza hofu yao kuhusu kuongezeka kwa vurugu na kuuawa kwa waandamanaji nchini Sudan ambao wamekuwa wakipinga ongezeko la bei ya bidhaa na uhaba wa mafuta na chakula. Arnold Kayanda na maelezo zaidi.
Mtaalamu huyo amesema anahofu sana na taarifa ya kwamba vikosi vya serikali vinatumia silaha za moto wakati wa maandamano yaliyogubika nchi hiyo tangu tarehe 19 mwezi huu wa Desemba.
Amesema serikali inapaswa kuyafanyia kazi malalamiko ya kweli ya watu wa Sudan.
Watalaamu hao wa Umoja wa mataifa pia wamezungumzia ripoti kuhusu kukamamatwa na kutiwa kizuizini kwa idadi isiyofahamika ya waandamanaji wakiwemo wanafunzi na wanaharakati wa siasa.
Wamesihi mamlaka za Sudan ziwaachie huru wale wanaoshikiliwa na ufanyike uchunguzi huru na kuhakikisha vikosi vya usalama vinadhibiti maandamano kwa kuzingatia makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Watalaamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema wako tayari kushirikiana na mamlaka za Sudan na wadau wake katika kuweka mazingira ambayo yanazingatia haki za binadamu na utawala wa kisheria na wameahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Sudan.