Ndoto zangu kupinga matumizi ya plastiki sio za abunuwasi:Wakibia

27 Disemba 2018

Mwaka 2018 unapofikia ukingoni tunarejelea baadhi ya taarifa ambazo tulizitangaza na tunaamini kuwa zilikuwa na umuhimu mkubwa na miongoni mwao ni ile ya mwanaharakati wa mazingira kutoka Kenya James Wakibia.

Mwezi Juni mwaka huu wakati wa siku ya baharí duniani, iliyokuwa na kaulimbiu kuzuia matumizi ya plastiki na kuhamasisha hatua za kuwa na baharí salama, Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa haikusita kuzungumza na James Wakibia mwanaharakati wa mazingira kutoka  Kenya ambaye kwa miaka sita sasa amekuwa akipigia chepuo harakati za kuondokana na plastiki siyo tu nchini  mwake bali pia dunia nzima kwa  ujumla.

Katika ripoti yetu iliyotangazwa tarehe 8 mwezi Juni mwaka huu tulimuuliza Bwana Wakibia alijisikia vipi kampeni yake sasa kufikia ngazi  ya kimataifa?

“Nahisi vizuri sana kwamba kazi  yangu imemulikwa na imechukuliwa na Umoaj wa Mataifa kwa sababu nchi nyingi sasa zitasikia hili neno kuhusu  kupinga marufuku ya plastiki.”

Umoja wa Mataifa unasema kuwa chembe chembe za plastiki zilizoko baharini ni nyingi sana na itafikia wakati kiwango cha plastiki baharini kitakuwa ni kikubwa kuliko samaki na je Wakibia  anadhani hatua zipi zinapaswa kuchukuliwa changamoto hiyo.

Naomba serikali zote hasa za Jumuiya ya Afrika Mashariki zianze na kuweka mikakati ya kupi marufuku hizi plastiki, na pia aina nyingine za plastiki ambazo zinatumika mara moja kama vile mirija, vikombe vya palstini na hivi vijiko vya plastiki na aina nyingine ya plastiki ambazo hutumika mara moja.”

Bwana Wakibia amekuwa akiendesha kampeni yake ya kulinda na kuhifadhi mazingira kwa njia mbili ambapo mosi  ni kukusanya taka hizo za plastiki na kisha kuzichoma na pili kuandika makala mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kuhusu taka hizo kwa lengo kuwachagiza wananchi kuachana na matumizi ya plastiki.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud