Waliokufa Indonesia kutokana na Tsunami sasa ni 281- OCHA
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na tsunami iliyokumba maeneo ya mwambao mwa kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia sasa imefikia 281 na wengine zaidi ya 1,000 wamejeruhiwa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya dharura, OCHA imesema pamoja na idadi hiyo ya vifo na majeruhi, hadi sasa watu 57 hawajulikani waliko huku wengine takribani 11,700 wamepoteza makazi yao.
Ikinukuu shirika la kitaifa la Indonesia linalishughulikia majanga-BNPB, OCHA imesema pamoja na madhara ya tsunami hiyo kwa binadamu, baadhi ya miundombinu na majengo vimeharibiwa, zikiwemo nyumba 611, hoteli 69, maduka 60 na mashua 420.
Tsunami hiyo ilipiga Indonesia Jumamosi na inasadikiwa chanzo ni maporomoko ya ardhi ndani bahari yaliyochochewa na mlipuko wa volkano ya Anak Krakatau katika eneo la mlango wa bahari wa Sunda.
Wimbi hilo kubwa la Tsunami liliathiri zaidi wilaya za Pandegland na Serang zilizoko katika mkoa wa Banten na pia wilaya zingine mbili katika mkoa wa Lampung kwenye kisiwa cha Sumatra.
Vikosi vya usalama na mashirika mbalimbali ya ndani mwa nchi hiyo vinaendelea kutoa msaada.
Hadi sasa serikali haijaomba msaada ingawa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika salamu zake za rambirambi kwa serikali ya Indonesia mwishoni mwa juma, amesema kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa usaidizi iwapo utaombwa kufanya hivyo.