Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNSOM yalaani mashambulio mjini Mogadishu

Magari  yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.
UN /Stuart Price
Magari yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.

UNSOM yalaani mashambulio mjini Mogadishu

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Haysom amelaani mashambulio mawili ya leo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu ambayo yamesababisha vifo vya watu wapatao 20 na wengine wamejeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa leo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, UNSOM imesema shambulio la kwanza limetokea katika kizuizi cha barabarani karibu na jumba la Sanaa la kitaifa mjini Mogadishu ambapo miongoni mwa waliouawa ni mwandishi wa habari mwenye asili ya kisomali anayefanya kazi na televisheni ya Universal Network yenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza.


Imeripotiwa kuwa shambulio la pili lilitokea karibu na eneo hilo wakati waokoaji na magari ya wagonjwa yalipokuwa yanasogelea eneo la shambulio la kwanza, ambapo tayari kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kimekiri kuhusika na mashambulio hayo.


Haysom ambaye pia ni mkuu wa UNSOM amenukuliwa kwenye taarifa akisema kuwa, “shambulio la Mogadishu ni ishara nyingine ya woga dhidi ya wananchi wa Somalia na haki yao ya msingi ya kuishi kwa amani na utu.Tunaihimiza serikali ya Somalia ifanye kila juhudi katika vita vyake dhidi ya mawakala wa misimamo mikali ambao wanawajibika kwa uhalifu huu wa kikatili.”


Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametuma salamu za rambirambi kwa familia na marafiki wa walioathiriwa na shambulio hilo na kuwatakia majeruhiwa ahueni ya haraka.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.