Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na AU zaungana kuondokana na  jembe la mkono Afrika

Mkulima  akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.
Photo: FAO/Giulio Napolitano
Mkulima akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.

FAO na AU zaungana kuondokana na  jembe la mkono Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kwa kushirikiana na Muungano wa Afrika, AU wameandaa mfumo utakaowezesha kuzindua kilimo cha kutumia zana za kisasa za kilimo barani Afrika ili kuondokana na kilimo cha jembe la mkono na hivyo hatimaye kuongeza tija na kuvutia vijana kwenye sekta hiyo. 

FAO na AU wanasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wakulima katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanatumia zana za mkono kama vile majembe na mapanga, hali inayosababisha Afrika kuwa eneo ambalo kiwango cha mavuno kwa hekta moja kuwa cha chini zaidi.

Akihojiwa katika mfululizo wa vipindi vya FAO vyenye lengo la kusaka mbinu za kutokomeza njaa duniani, Mhandisi wa kilimo FAO Joseph Mpagalile anasema kilimo cha zana za kisasa ni zaidi ya kutumia trekta.

“Inahusisha uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa vifaa na zana za kilimo ambazo mkulima anaweza kutumia ili kufanya kazi yake iwe rahisi, kuongeza tija na  ufanisi wa kazi yake.”

AU inasema kuwa matumizi ya zana za kisasa yatawezesha wanawake pia kuongeza tija kwenye kilimo halikadhalika vijana ambao sasa hivi wengi wao wanakwepa kilimo kutokana na zana duni ambapo Bwana Mpagalile anasema..

“Vijana wanaweza kutumia mathalani simu ya kiganjani kuendesha baadhi ya mashine za shambani, kuagiza mashine ndogo iletwe shambani kufanya  kazi kupitia huduma za kukodi na hii ni jambo zuri sana.”

AU na FAO wanasema mfumo huo mpya unashirikisha zaidi sekta binafsi na ushiriki wa sekta hiyo utakuwa na mafanikio iwapo kutakuwepo na mazingira bora ya kuifanya iwe na faida sambamba na kufanikisha mikopo kwa wakulima wadogo ili waweze kupata zana za kisasa za kilimo.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.