Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ardhi imesalia kuwa mkombozi wangu- Mkulima Somalia

Ismail Isack Amin, mkulima mwenye umri wa miaka 66 ambaye anasema amekuwa akijinufaisha na ardhi  yenye rutuba nchini mwake Somalia tangu akiwa na umri wa miaka
UNSOM video screen capture
Ismail Isack Amin, mkulima mwenye umri wa miaka 66 ambaye anasema amekuwa akijinufaisha na ardhi yenye rutuba nchini mwake Somalia tangu akiwa na umri wa miaka

Ardhi imesalia kuwa mkombozi wangu- Mkulima Somalia

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Somalia, harakati za kuhakikisha wananchi wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kuzaa matunda kwa wananchi ambapo ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini  humo, UNSOM inadhihirisha juhudi hizo kupitia mfululizo wa video zinazonesha wananchi wakishiriki harakati mbalimbali. 

Sauti ya Ismail Isack Amin, al maaruf, Sharif Ismail, anasema yeye ni mkulima mkazi wa Baidoa lakini mashamba yake yapo eneo la mashambani liitwalo Misko.

Katika mfululizo wa video zilizoandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM zikipatiwa jina ‘Sauti za Somalia’ kwa lengo la kuonesha harakati za kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, biashara, elimu na afya, tunakutana na mkulima Ismail.

Yeye anasema alianza shughuli za kilimo akiwa na  umri wa miaka 14 na sasa ana umri wa miaka 66 na ndio tegemeo lake kuu na akiwa shambani mwake Ismail anasema..

“Napenda kazi hii kwa sababu ndio tegemeo la damu na mwili wangu na ninanufaika kiafya kutokana na lishe ya mtama ninaovuna. Napenda kunufaika na jasho langu, kulima ardhi aliyonipatia Mungu na kutumia kwa manufaa yangu.”

Mkulima huyu wa Baidoa nchini Somalia ambaye nyumbani mwake anaonekana kuwa ni mfugaji pia wa kuku, anasema yeye hulima maharage, mahindi na mtama na anapata faida .

“Faida ni akiba yangu, akiba ambayo naweza kutumia kununua mifugo na chochote ninachotaka. Kinachosalia naweza kutumia kwa kile ninachotaka kwa maisha yangu.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.