Madhila kwa Wahamiaji na wakimbizi wanaopitia Libya haisemeki-UN

20 Disemba 2018

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Tripoli imesema wahamiaji na wakimbizi wanakabiliwa na hofu na madhila yasitopimika tangu wanapoingia nchini Libya, muda wote wanaoishi katika nchi hiyo na ikiwa watafanikiwa kusogea mbele katika harakati zao za kujaribu kuvuka bahari ya Mediteranea.

 

Ripoti hiyo yenye kurasa 61 ikiwa imechapishwa kwa ushirikiano wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na haki za binadamu imeangazia kipindi cha miezi 20 nyuma hadi kufikia mezi Agosti mwaka huu wa 2018 ikionesha kwa kina ukiukwaji mkubwa na manyanyaso yanayofanywa na maafisa wa serikali, makundi yenye silaha, waporaji na wasafirishaji haramu wa wahamiaji na wakimbizi. Matendo hayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu ni pamoja na mauaji, mateso, kuwaweka watu vizuizini, ubakaji, utumwa na kuwafanyisha kazi kimabavu.

Kwa kutumia visa 1300 ambavyo vimefuatiliwa na watu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kwenyewe na kwa wahamiaji ambao wamerejea Nigeria au wamefika Italia, ripoti inafuatilia safari nzima ya wahamiaji na wakimbizi kutoka mpaka wa kusini wa Libya, kupitiajangwani hadi pwani ya kaskazini, safari ambayo inakabiliwa na hatari kubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kila hatua inayopigwa njiani humo.

Ripoti imeendelea kueleza kuwa wanawake wengi na wasichana waliohojiwa na UNSMIL wameripoti kubakwa na wahalifu, wavamizi na wasafirishaji haramu. Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliotembelea vituo 11 ambako maelfu ya wahamiaji na wakimbizi wanashikiliwa, walikusanya Ushahidi wa mateso, unyanyasaji, utumikishwaji na ubakwaji unaofanywa na walinzi na wameripoti kuwa wanawake mara nyingi wanawekwa katika maeneo ambayo hakuna walinzi wa kike hali ambayo inaongeza uwezekano wa hatari ya kubakwa na kufanyiwa manyanyaso mengine. Mara nyingi wanawake wanaoshikiliwa hulazimika kufanyiwa ukaguzi wakiwa bila nguo huku wakitizamwa na walinzi wanaume.

Wale ambao wanafanikiwa kujaribu kuvuka bahari ya Mediterania, hukamatwa na walinzi wa Pwani ya Libya na kisha hurejeshwa Libya ambako wanarudishwa katika mateso waliyoyatoroka.

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Michelle Bachelet akizungumzia kinachoendelea nchini Libya amesema, “Hali hiyo ni mbaya na ya kutisha”

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter