Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC Jiepusheni na uhalifu wakati wa uchaguzi la sivyo mtawajibishwa- ICC

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya  ICC
UN Photo/Rick Bajornas)
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya ICC

DRC Jiepusheni na uhalifu wakati wa uchaguzi la sivyo mtawajibishwa- ICC

Amani na Usalama

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC tarehe 23 mwezi huu, mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC imeonya kuwa yeyote yule nchini humo ambaye atachochea, ama atashiriki katika fujo kwa kuamuru, kutaka ama kuhimiza au kuchangia kwa njia yoyote ile au kutenda makosa yaliyo chini ya mamlaka ya ICC atashtakiwa na kufikishwa mbele ya mahakama. 

Onyo hilo limetolewa leo na mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda, katika taarifa yake aliyotoa leo mjini The Hague, Uholanzi wakati huu ambapo DRC inajiandaa kwa uchaguzi wa rais, magavana, wabunge na madiwani.

Bi. Bensouda amesema hatua yake inafuatia wasiwasi mkubwa kutokana na hali kuwa tete na ongezeko la fujo jambo ambalo linaweza  kusababisha kuibuka kwa makosa makubwa ambayo yanajumulishwa kati ya  yale mahakama ya ICC inayoyashughulikia.”

Amesema DRC ni mwanachama wa mkataba wa Roma ulioanzisha ICC, na mahakama yenyewe iliundwa  kuwafungulia mashtaka wale ambao  wameshtumiwa kutenda makosa mabaya kwa mujibu wa jamii ya kimataifa ambayo ni :mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu,na uhalifu wa kivita.

Bi. Bensouda amesema kuwa uzoefu katika nchi zingine unaonyesha iwapo jazba ikipanda wakati wa kampeni za uchaguzi na watu wasipojizuia, hilo linaweza kusababisha makosa ambayo yanashughulikiwa na ICC.

Halikadhalika amewakumbusha viongozi wa kisiasa kuwa wanawajibika kuhakikisha kuwa  mchakato mzima wa uchaguzi unaendelea kwa utulivu na kuwataka wafuasi wao kujizuia kufanya fujo, kabla, wakati na baada ya chaguzi hizo, akisema ofisi yake itaendeleakufuatilia hali ilivyo nchini humo na kuwajibika ipasavyo na kukariri wito wake kwa watu wa DRC hususan  watawala, wanasiasa,wafuasi wao, kufanya kila wawezalo kuepusha na kuzia  vitendo vya fujo popote pale na wakati wowote ule.