Tushikamane kwa maslahi na utu wa kila mtu

20 Disemba 2018

Leo ni siku ya kimataifa ya mshikamano ambapo Umoja wa Mataifa unataka kila mtu popote pale alipo ashikamane na mwenzake ili kurejesha imani iliyopotea na kusongesha utu wa kila mtu, ili hatimaye kuweza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kupitia video maalum iliyoandaliwa na  shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake, UN-Women, suala la mshikamano na wanawake, wasichana na watoto wa kike linapatiwa kipaumbele ambapo viongozi mbalimbali wa umoja huo akiwemo Katibu Mkuu Antonio Guterres na Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka wanapaza sauti za mshikamano.

Mathalani Bwana Guterres anasema “mustakabali wetu unategemea mshikamano,” ilhali Bi. Ngucka anatoa wito kwa wavulana wote kujiunga na kampeni ya wanaume kusimama kidete kutetea wanawake ijulikanayo kama HeForShe.

Wengine katika video hiyo ni Katibu Mkuu wa shirika la skauti duniani, Ahmad Alhendawi ambaye anasisitiza mshimano wake na skauti wote milioni 50 duniani. 

Waigizaji nao hakuwabaki nyuma wakipazia sauti za mshikamano na watoto wao wa kike, wengine wakitaja wahandisi wa kike wakisema “ukweli ni kwamba tunakuwa na nguvu zaidi tukiwa pamoja na katika siku ya mshikamano nasimamia usawa wa kijinsia. Tunasimamia pamoja usawa kwa mamilioni ya wasichana duniani kote ambao wako kwenye skauti.”

Na mwishoni wanahoji, “wewe je?”

Siku ya mshikamano duniani ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 22 mwezi Desemba mwaka 2005 kupitia azimio namba 60/209.

Azimio hilo lilitambua mshikamano kama moja ya maadili ya msingi duniani ambayo yanapaswa kuwa msingi wa uhusiano baina ya watu katika karne ya 21.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter