Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yainua wakulima wadogo wadogo Tanzania kwa kuwapa stadi za kilimo

Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na  hivyo kuinua kipato cha wakulima.
UNDP Uganda/Luke McPake
Miradi ya FAO ya kuwawezesha wakulima kama hawa kupata stadi za kilimo bora, inaongeza uzalishaji na hivyo kuinua kipato cha wakulima.

FAO yainua wakulima wadogo wadogo Tanzania kwa kuwapa stadi za kilimo

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Chakula na kilimo duniani FAO kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania wameungana kutelekeza mradi wa kuwafundisha wakulima wadogowadogo stadi za kilimo bora. Tayari zaidi ya wataalam 1000 wanaofanya kazi katika zaidi ya wilaya 137 nchini Tanzania wamefundishwa stadi hizo katika Chuo cha wakulima cha Mkindo kilichoko Morogoro. 

Chuo hiki cha wakulima Mkindo mkoani Morogoro nchini Tanzania kilianzishwa mwaka 1996 kupitia ushirikiano wa Tanzania, FAO na Indonesia chini ya mpango wa ushirikiano wa nchi za kusini.

Mashamba darasa ya mwanzo yalitumika kuanzisha aina mpya ya mpunga na teknolojia ya umwagiliaji ili kuongeza wastani wa uzalishaji wa mchele nchini Tanzania kutoka tani 2 hadi 6 kwa hekta.

Dkt. Moses Temi wa Chuo cha wakulima Mkindo anasema,“Tulipoanzisha mafunzo hapa miaka 16 iliyopita, tulianza na wakulima 100 ili waongeze uzalishaji na pia wawafundishe wakulima wengine katika Kijiji hiki na pia katika vijiji jirani. Idadi ya sasa ya wakulima tulio nao ni elfu tatu ambao wanazalisha tani 6 hadi 7 kwa hekta. Muundo huu umechukuliwa na serikali kama mafanikio na umehusishwa katika programu mbalimbali za kilimo”

Kilomita kadhaa kutoko chuo hiki ni kijiji cha Ujamaa cha Msolwa ambako kuna kundi la vijana la Maendeleo ambao kwa awali walitumia fedha zao kuanzisha shamba lao la mpunga na baada ya kuhitimu masomo katika Chuo cha Mkindo, wameanzisha shamba lingine kama anavyoeleza Peter Njechele mmoja wa wakulima hao vijana,“Mwanzo tulipoanza shamba hili tulikuwa hatujapewa fedha ya kuanzia kutoka kwenye mradi, baadaye shirika la FAO likatuwezesha kupata fedha za kuweza kufanya shughuli hizi za kilimo. Kwa hiyo tumeona kwa kuwa eneo hili vado hatujavuna tutafute eneo lingine ili kusudi tuweze kuanzisha shughuli hiyo”

Zaidi ya wataalamu 1000 wa kilimo wamepata mafunzo tangu kuanzishwa kwa chuo hiki na ni wataalamu kutoka ngazi ya kijiji hadi taifa. Takribani kila wilaya nchini Tanzania ina mtaalam mmoja aliyepata mafunzo kutoka Chuo cha wakulima cha Mkindo.

Tweet URL

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.