Uwepo wa mahandaki kutoka Lebanon hadi Israel kunatia wasiwasi mkubwa-Lacroix

19 Disemba 2018

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amesema mahandaki yaliyochimbwa kuanzia Lebanon hadi Israel ni suala la wasiwasi mkubwa na ni ukiukaji wa azimio namba 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo jijini New  York, Marekani, kilichokutana kuangazia hali Mashariki ya Kati, Lacroix amesema wasiwasi huo unatokana na taarifa kutoka ujumbe wa umoja huo  nchini Lebanon, UNIFIL ambao umethibitisha uwepo wa mahandaki manne kusini mwa Lebanon, huku mawili yakipita eneo lisilo la mapigano au Blue Line ambalo ni la mpaka na Israel, ingawa mahandaki hayo hayana sehemu ya kutokea upande wa Israel.

Kwa hivyo amesema Umoja wa Mataifa umetaka mamlaka za Lebanon kuchukua hatua za haraka kwa mujibu wa azimio namba 1701 na zishirikiane na UNIFIL katika kutambua na kusambaratisha mahandaki yoyote yanayovuka mpaka kutoka Lebanon.

Kwa upande wake Mwakilishi wa kudumu wa Lebanon kwenye Umoja wa Mataifa, balozi Amal Mudallai amesema mjadala wa Baraza la Usalma kuhusu Lebanon unakumbusha nyakati ambazo Israel iliingilia na kukalia maeneo ya Lebanon na hivyo akahoji iwapo hayo ni mashambulizi mapya.

Balozi Amal Mudallali, Mwakilishi wa kudumu wa Lebanon kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama Jumatano Desemba 19, 2018
UN /Evan Schneider
Balozi Amal Mudallali, Mwakilishi wa kudumu wa Lebanon kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama Jumatano Desemba 19, 2018

Amesema kuwa Israel imekiuka azimio 1701 na uhuru wa Lebanon mara 1,800 kwa mwaka na kuingilia maeneo yake ya nga mara 84 kwa siku katika kipindi cha miezi minne iliyopita pekee.

Balozi Mudallai, ameongeza kuwa kama Lebanon ingaliitisha kikao cha Baraza la Usalama, kila Israel inapokiuka uhuru wa Lebanon tangu 2006,"mngalikuwepo hapa saa 24 kwa wiki kuyajadili."

Mwakilishi huyo wa Lebanon ameonesha wasiwasi wa kuwepo kwa upendeleo ambapo ripoti za nchi yake kuhusu ukiukaji wa uhuru wake kama nchi zinawekwa kwenye kumbukumbu ilhali malalamiko ya Israel yanasababisha Baraza la Usalama kukutana na vitendo vya Israel haviwajibishwi.

Balozi Danny Danon, Mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama Jumatano tarehe 19 Desemba 2018 kwenye kikao kuhusu Mashariki ya Kati.
UN /Eskinder Debebe
Balozi Danny Danon, Mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama Jumatano tarehe 19 Desemba 2018 kwenye kikao kuhusu Mashariki ya Kati.

Akijibu hoja hizo, mwakilishi wa kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa wa Israel, Balozi Danny Danon amesema nchi yake imefuatilia mradi wa mahandaki wa Hizbollah kupitia vyombo vya upelelezi na kusema operesheni ya kujikinga ya Kasakazini ni mpango wa kujilinda dhidi ya shambulizi.

Ameongeza kundi hilo lililojihami nchini Lebanon lina karabati handaki la ukatili kutoka mji wa Lebanon wa Kfarkila hadi Israel, na kuhoji wajumbe wafikirie kile kitakachofanyika kwa kijiji hicho iwapo watalazimika kujikinga.

Balozi Dannon amesema Hizbollah wanashikilia taifa la Lebanon ili kushambulia Israel na serikali ya Lebanon imewaachia na kufumba macho wakati raia wake wakiishi katika hali ya ndani ya bomu linalotarajiwa kulipuka wakati wowote na kwamba Lebanon imewatelekeza watu wake.

Azimio 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa mwaka 2006 ili kutatua mzozo kati ya Lebanon na Israel.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter