Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu waighubika DRC:UN Ripoti

Mlinda amani kutoka India akifanya doria huko Kashugu, Kivu Kaskazini ili kuwahakikishia usalama wananchi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi.
MONUSCO/Force
Mlinda amani kutoka India akifanya doria huko Kashugu, Kivu Kaskazini ili kuwahakikishia usalama wananchi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi.

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu waighubika DRC:UN Ripoti

Haki za binadamu

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa leo inaonyesha kuendelea kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ikiwemo mauaji ya mamia ya watu, visa vya utesaji na ukatili wa kingono dhidi ya raia katika kipindi cha miaka miwili  iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo usalama na hali ya kibinadamu katika eneo la Kivu ya Kaskazini vilizorota kati ya Januari 2017 na Oktoba 2018 huku idadi ya visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili vikifikia theluthi moja ya viza vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyoorodheshwa nchi nzima.

Hali ya kuongezeka kwa idadi ya makundi yenye silaha ambayo yanapigana na vikjosi vya usalama vya serikali na wenyewe kwa wenyewe ili kupata udhibiti wa maeneo au maliasili ndio imeelezwa kuwa sababu ya kuzorota kwa hali nchini humo.

Ripoti hii ilitochapishwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa , imejikita katika hali sugu inayotamalaki Masisi na Lubero maeneo ambako Umoja wa Mataifa umeorodhesha takriban visa 324 vya mauaji , waathirika 832 wa utesaji au ukatili, waathirika 173 wa ubakaji  au ukatili wa kingono (wanawake 114, watoto 58 na mwanaume 1) na visa 431 vya utumikishwaji wa shuruti.

Ripoti hiyo imesema kwa ukiukwaji wote huu na changamoto za usalama waathirika wakubwa ni raia.

Tangu mwaka 2015 idadi ya visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu imekuwa ikiongezeka katika majimbo hayo ambapo wanawake na watoto wamekuwa wakitekwa kila wakati kwa ajili ya kutumiwa kingono, visa vya ukakaji na ubakaji wa magenge ukifanywa na pande zote katika mzozo  yaani jeshi la serikali ya (FARDC) na makundi yenye silaha, huku ripoti ikiongeza kwamba watoto pia hushinikizwa kuingia jeshini kama askari watoto.

Akisisitiza haja ya kukomesha ukiukwaji huo wa haki za binadamu DRC, kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Michelle Bachelet amesema “Juhudi zote lazima zifanyike ili kuwalinda raia hususani wasiojiweza na kuzuia uhalifu huo kuendelea. Katika baadhi ya vijiji kwa mfano Masisi na Lubero ukatili wa kingono unatumika kwa njia mbaya sana na baadhi ya makundi ili kuziadhibu na kuzitisha jamii”

Ripoti pia imebainisha ni jinsi gani kutapakaa kwa ghasia kumesababisha watu wengi kutawanywa na wengi wa watu hao wanavyoishi katika mazingira magumu na yenye ghasia.

Ripoti hiyo iliyoandikwa kutokana na taarifa zilizokusanywa na maafisa wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, inasema kwamba makundi yenye silaha yanawajibika kwa theluthi mbili ya visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukaliti ulioorodheshwa wakati wa kipindi hiyo cha miaka miwili, huku vikosi vya usalama vya serikali hasa jeshi na polisi vikiwajibika kwa theluthi moja ya ukiukwaji huo,ambapo aslimia 20 vimetekelezwa na jeshi na asilimia 9 polisi ya nchi hiyo.

Naye mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo , MONUSCO ambaye pia ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu BI. Leila Zerrougui amesema “ bila kuwepo uchunguzi wa uhakika kubaini uwajibikaji kwa kila uhalifu na bila hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa uhalifu huo , haijalishi nani ametekeleza ukiukwaji huo kwani ukwepaji sharia utaendelea na raia wataendelea kuwa katikati ya mapambano baiana ya makundi yenye silaha na vikosi vya serikali pande ambazo zilistahili kuwalinda.”

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.