Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata kulazimu WFP kukata msaada kwa baadhi ya wapalestina mwakani: WFP

Misaada ya kibinadamu ni tegemeo kubwa kwa wapalestina, pichani mtoto akilinda vyema msaada kutoka UNRWA
2013 UNRWA/Shareef Sarhan
Misaada ya kibinadamu ni tegemeo kubwa kwa wapalestina, pichani mtoto akilinda vyema msaada kutoka UNRWA

Ukata kulazimu WFP kukata msaada kwa baadhi ya wapalestina mwakani: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP linasaka  dola milioni 57  ili liweze kuendelea  kutoa msaada mwaka ujao kwa  wapalestina 360,000 wanaoishi ukanda wa Gaza na ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Yerusalam inasema hatua hiyo inafuatia ukata unaokabili shirika hilo ambao unaweza kuathiri watu maskini 193,000 katika maeneo hayo.

WFP inasema kipaumbele cha WFP kinategemea uwepo wa fedha na watu 27,000 katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan huenda wasipate tena  msaada zaidi huku waliosalia watapatiwa asilimia 80 tu ya mgao wao wa  kila mwezi.

WFP ina wasiwasi kuwa ukata utaathiri vibaya  upatikanaji wa wa chakula, maisha na maslahi ya watu inayowasaidia katika maeneo hayo ya wapalestina.

Mwakilishi wa WFP katika eneo la Palestina, Stephen Kearney, anasema kuwa, “msaada wa WFP umekuwa mkombozi kwa maelfu ya watu  ambao wamepungukiwa na walichonacho wakijaribu kukabiliana na maisha magumu. Pengo lililoko kati ya mahitaji ya chakula yanayoongezeka na huku vitndeakazi vikipungua, hii inalazimu WFP ichukue uamuzi mgumu.”

WAKAZI WENGI WA GAZA NA UKINGO WA MAGHARIBI MWA MTO JORDAN TEGEMEO LAO NI MISAADA

WFP inasema kuwa wasiwasi wa kutokuwepo  kwa chakula unazidi kuongezeka, ukiathiri theluthi moja ya idadi yote ya wapalestina na hali mbaya inapatikana  ukanda wa Gaza ambako takriban asilimia70 watu kwenye eneo hilo wana shaka iwapo watapata chakula au la, hii ikiwa ni kutokana na matokeo ya uchunguzi wa kitaifa  uliofanywa  juzi kuhusu uwepo wa chakula.

Msaada wa WFP kawaida ni kwa watu maskini na jamii ambazo hazipati chakula.

Wengi wao wanajitahidi kuishi kwa kiwango cha chini ya dola moja kwa siku na hawawezi kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, nguo na pia mahitaji ya makazi.

Kwa mantiki hiyo, kukata msaada na mgao wa chakula kutawalazimisha kukosa chakula na pia kupata madeni zaidi na watoto wao hawataenda shuleni.

WFP inasema hali hiyo inaweza kuchochea mgogoro wa  kibinadamu pamoja na hali isiyokuwa salama katika eneo la Gaza.

Bwana Kearney amesihi jamii ya kimataifa na wahisani waimarishe msaada wao ili kuzuia hali ngumu zaidi miongoni mwa wapalestina.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.