Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaomba zaidi ya dola bilioni 2 kukidhi mahitaji katika mgogoro mkubwa kabisa barani Afrika

Matatizo ya muda mrefu yamesababisha mateso makubwa kwa watu wa Sudan Kusini hasa  wanawake.
UN Photo/Isaac Billy
Matatizo ya muda mrefu yamesababisha mateso makubwa kwa watu wa Sudan Kusini hasa wanawake.

UNHCR yaomba zaidi ya dola bilioni 2 kukidhi mahitaji katika mgogoro mkubwa kabisa barani Afrika

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR linasema linahitaji dola bilioni 2.7 ili kuweza kufanikisha huduma zake za kutoa misaada kwa mamilioni ya wakimbizi wa Sudan Kusini walioko  ndani  na nchi jirani katika kipindi cha mwaka 2019 na 2020.

UNHCR pamoja na wadau wengine wa misaada wamezindua ombi hilo ili kuhakikisha mahitaji ya msingi ya wakimbizi milioni 4  wa Sudan kusini yanapatikana

Akizungumza na waandishi habari hii leo mjini Geneva Uswisi, msemaji wa UNHCR,Charlie Yaxley amesema kipaumbele cha UNHCR kuhusu wakimbizi hao,

“Ni kuendeleza mipango ya kuhimiza kuishi kwa pamoja kati ya wakimbizi na jamii zinazowapa hifadhi ili kuhakikisha kuwa jamii hizo zinaishi pamoja kwa amani. Katika hali yoyote ya ukimbizi ni muhimu kuhakikisha kuwa jamii zote zinasaidiwa.”

Ameongeza kuwa kinacholitia hofu zaidi shirika hilo ni 

“Unyanyasaji wa kijinsia na kingono pamoja na ulinzi wa watoto ndio wasiwasi tulionao kwani asilimia 83 ya wakimbizi ni wanawake na watoto. Wanawake wengi wameripoti visa vya kubakwa pamoja unyanyasaji wa aina tofauti wa kingono na kijinsia, mbali na waume zao kuuawa, na pia kutekwa kwa watoto wakati wanakimbia.”

 UNHCR inasema miaka mitano tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka watu zaidi ya milioni 2.2 wamekimbilia nchi sita jirani ambazo ni Uganda, Sudan,Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo-DRC pamoja na Jamhuri ya Afrika ya kati. Pia na wengine milioni 1.9 wamebaki kuwa wakimbizi ndani nchini mwao.  

Ingawa visa vya mapigano vimepungua  katika sehemu kadhaa za nchi hiyo, tangu kutiwa saini mkataba wa amani Septemba  2018 jambo ambalo UNHCR inalifurahia, pia inaomba  pande zote husika  kuheshimu na vilevile   kutekeleza makubaliano hayo. 

Hata hivyo inasema kutokana na historia  ya kutoheshimu juhudi za amani za awali UNHCR inaona mazingira ya sasa si salama kwa wakimbizi wa Sudan Kusini kurejea nyumbani wakati huu.

Mbali na hayo UNHCR inasema hali kwa wakimbizi bado ni ni mbaya ikitoa mfano wa shule  hazina waalimu pamoja na vitendeakazi hali ambayo inawafanya nusu ya watoto wa Sudan Kusini ambao ni wakimbizi kuacha masomo. 

Upande wa huduma za afya UNHCR inasema zahanati zilizopo hazina madaktari, au wauguzi pamoja na dawa na ufadhili mdogo umesababisha kupunguza mgao wa chakula nchini Ethiopia huku nchini Sudan baadhi ya wakimbizi na jamii zinazowakaribisha wamekuwa wakitumia lita tano za  maji kwa siku kwa kila mtu jambo ambalo linasababisha hali kuwa ngumu zaidi.

Hivyo UNHCR inawasihi wahisani kusaidia kifedha kwa ajili ya mustakabali wa wakimbizi hao kwani mwaka 2018 pamoja na washirika wake walipata asilimia 38 ya pesa zilizoombwa za dola milioni1.4 ili kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.